Johnson agoma kujiuzulu baada ya pigo la mahakama ya juu
24 Septemba 2019Uamuzi huo wa mahakama ya juu zaidi nchini Uingereza umeungwa mkono kwa kauli moja na majaji wake wote 11, hali ambayo inazidisha uzito wa uamuzi huo, na matatizo kwa waziri mkuu Boris Johnson. Rais wa mahakama hiyo hiyo, Lady Hale amesema hatua ya serikali ilikuwa na malengo ya kulitatiza bunge kufanya majukumu yake.
''Kwa hiyo mahakama imehitimisha kwamba uamuzi wa kumshauri Malkia kusitisha shughuli za bunge ulikuwa kinyume na sheria, kwa sababu matokeo yake yalilitatiza bunge, au yalilizuia bunge kufanya majukumu yake ya kikatiba, bila sababu yoyote ya msingi.'' Amesema rais huyo wa mahakama ya juu ya Uingereza.
Johnson ajikaza kisabuni
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya uamuzi huo wa mahakama mjini London, Boris Johnson ambaye yuko mjini New York akihudhuria Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, amepuuza miito iliyotolewa na wanasiasa mbali mbali wakimtaka ajiuzulu, akisema kuwa kwa maoni yake, uamuzi wa mahakama ya juu haukuwa sahihi.
Amesema, ''Inabidi niseme kwamba napingana vikali na uamuzi wa majaji. Sidhani kama ni sahihi, lakini bila shaka tutasonga mbele, na vikao vya bunge vitafanyika tena.''
Katika hukumu yake, mahakama ya juu imesema hivi sasa ni wajibu wa viongozi wa bunge kuamua muda wa kuanza tena vikao vyao, na tayari spika wa baraza la chini John Bercow, amesema milango ya bunge huko Westminster itafunguliwa kesho Jumatano.
Spika huyo amesema uamuzi wa mahakama ya juu ni wa kihistoria, na kwamba raia wanayo haki ya kuona wawakilishi wao wakitimiza majukumu yao ya kikatiba, ya kuishikiza serikali kuwajibika.
Miito ya kumtaka ajiuzulu yahanikiza
Miongoni mwa wanasiasa waliomtaka waziri mkuu Boris Johnson kujiuzulu ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, ambaye amemtuhumu Johnson kuidharau misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.
Waziri kiongozi wa Scotland, sehemu ya Uingereza yenye mamlaka ya ndani Nicola Sturgeon amekwenda mbali, na kusema ikiwa Johnson hatokuwa na ujasiri wa kujiuzulu mwenyewe, basi wabunge waungane na kumtimua madarakani.
Mratibu wa masuala ya Brexit katika bunge la Umoja wa Ulaya Guy Verhofstadt, amesema hatimaye, katika mvurugano wa Brexit, imedhihirika kuwa utawala wa sheria nchini Uingereza bado uko hai na wenye nguvu.
ape,afpe