Hali ya kisiasa yazidi kuwa ngumu Uingereza
30 Agosti 2019Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza Boris Johnson amesema waingereza walishaamua kuondoka katika Umoja wa Ulaya kupitia kura ya maoni iliyofanyika mwaka 2016 na wabunge waliahidi mara kadhaa kufanikisha uamuzi huo.
"Tukisitisha hatua ya Uingereza kujiondoa katika umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 tutaondoa imani ya watu wetu katika siasa zetu, tutaweka madhara makubwa katika vyama vyetu vikubwa vya kisiasa na hatutasamehewa kwa kutotimiza kile wananchi wanachokitaka," alisema Johnson alipohojiwa na televisheni ya Sky nchini Uingereza.
Wabunge wa upinzani pamoja na wabunge wengine kutoka chama cha Concervative anachotokea Waziri Mkuu Johnson wamesema wanataka kuanzisha mswada kupingaBrexitisiyokuwa na makubaliano, ambao utafiti wa serikali umeonya kuwa hilo likifanyika yani Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano kunahatarisha nchi hiyo kukabiliwa na uhaba wa chakula, madawa na mafuta.
Lakini Borris Johnson amesema kujitayarisha kuondoka bila makubaliano kutasababisha serikali kupata makubaliano ya kweli na Umoja huo.
Kesi ya kisheria ya kuzuwia uamuzi wa Johnson yaahirishwa
Siku ya Jumatano Waziri Mkuu huyo wa Uingereza alisitisha bunge wiki kadhaa kabla ya tarehe rasmi ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ili kuwazuwia wapinzani kuupinga mpango wake.
Hatua hiyo iliwashtua na kuwagadhabisha wabunge wanaotaka nchi hiyo kuondoka kwa makubaliano huku wengine wakiifananisha hatua hiyo na mapinduzi.
Huku hayo yakiarifiwa hii leo hatua ya kwanza ya kisheria ya kuzuwia uamuzi wa Boris Johnson wa kusitisha vikao vya bunge kufuatia mgogoro wa Brexit, imekhairishwa katika mahakama moja ya Scotland.
Jaji Raymond Doherty wa mahakama ya Edinburgh amesema kikao kamili cha kuisikiliza kesi hiyo kitafanyika Jumanne wiki ijayo uamuzi ambao umeongeza matumaini kwamba hatua ya serikali ya kusitisha bunge bado inaweza kuzuiliwa.
Vyanzo: afp,afp,reuters