Hali kuwa tata wabunge wa Uingereza wakikataa mkataba
18 Oktoba 2019
Makubaliano hayo yamepatikana baada ya takriban miaka mitatu ya kuvutana na wiki kadhaa kabla ya muda wa mwisho wa Oktoba 31 kwa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Kazi iliyosalia sasa ni ya bunge la Uingereza litakalo kuwa na kikao maalum cha bunge hapo kesho Jumamosi kupiga kura ya iwapo liidhinishe makubaliano hayo ya Brexit au la.
Hata hivyo mpango mpya wa Johnson unakabiliwa na upinzani katika bunge lililogawanyika huku wapinzani wake miongoni mwao kiongozi wa chama cha Leba Jeremy Corbyn, wakikataa mkataba huo baada ya kutangazwa, na kuahidi kuwachukulia hatua wabunge wa chama hicho watakaounga mkono makubaliano hayo.
Haya yanajiri huku viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiwa tayari leo kuidhinisha bejeti ya muda mrefu ya umoja huo katika siku ya pili ya mkutano wao wa kilele mjini Brussels huku kukiwa na hali ya kutoelewana kuhusu jinsi ya kushughulikia nakisi ya ufadhili unaohusiana na suala la Brexit, na kukiwa na masuala mapya yanayopaswa kupewa kipaumbele kama uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi.
Hii leo, viongozi hao pia watamuidhinisha rasmi aliyekuwa mkuu wa shirika la fedha duniani Christine Lagarde kama rais mpya wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya.
Rais mteule wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen ambaye pia alikuwa sehemu ya makubaliano hayo ataangaziwa zaidi huku wanachama wakizungumzia masuala yanayopaswa kupewa kipaumbele katika siku zijazo katika umoja huo ambayo yanajumuisha azma kubwa katika mabadiliko ya tabia nchi na jukumu thabiti la kimataifa la Umoja wa Ulaya.
Von der Leyen pia anatarajiwa kuulizwa maswali kuhusu shida aliyojipata nayo na bunge la Ulaya ambalo liliwakataa makamishna wake watatu kati ya makamishna 26. Kutokana na hali hiyo, kundi lake jipya halitaweza kuchukuwa hatamu za uongozi tarehe 1 Novemba kama ilivoyokuwa imepangwa.