1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamala ahimiza umoja na kuahidi kuwa rais wa Wamarekani wote

30 Oktoba 2024

Kamala Harris ametumia kile kilichoitwa 'hoja za kuhitimisha kampeni zake' kwa kuwakumbusha Wamarekani jinsi maisha yalivyokuwa chini ya Donald Trump. Zaidi ya watu 75,000 walihudhuria mkutano wake wa Washington.

https://p.dw.com/p/4mNln
Kamala Harris | Mgombea urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic
Harris amesema atawasikiliza Wamarekani wakati wote hata kama hawatompigia kuraPicha: Stephanie Scarbrough/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya umati mkubwa uliofurika katika bustani iliyoko karibu na Ikulu ya White House na Mnara wa Washington, Harris amesema atawasikiliza Wamarekani wakati wote hata kama hawatompigia kura.

Soma pia: Trump na Harris kuendelea na kampeni za mwisho mwisho

Alichagua eneo hilo la mjini Washington kwa sababu ndilo Mrepublican Trump alitumia kuuchochea umati uliovamia Jengo la Bunge mnamo Januari 6, 2021. Alisema Trump ametumia muongo mmoja uliopita akijaribu kuwagawanya Wamarekani, akiongeza kuwa rais huyo wa zamani anataka kurejea Ikulu ya White House sio kuyaangazia matatizo yao bali matatizo yake.

Timu ya Kampeni za Trump imejibu hotuba ya Harris ikiita kuwa ni ya kuirudisha nchi nyuma. Msemaji wa kampeni za Trump Karoline Leavitt amesema Kamala Harris anadanganya, kuchafua watu majina na kung'ang'ania yaliyopita ili kukwepa ukweli kwamba mgogoro wa wahamiaji, mfumko wa bei na vita vinavyotokota ulimwenguni vinatokana na sera zake mbovu.