1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kujulikana Alhamisi

22 Juni 2016

Kambi mbili pinzani nchini Uingereza, ile inayopiga kampeni ya nchi hiyo kubakia kwenye Umoja wa Ulaya na ile inayotaka ijiondoe, Jumatano zinakamilisha kampeni kabla ya wananchi kuamua katika kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/1JB9O
Picha: DW/J. Macfarlane

Akizungumza katika mahojiano yake ya mwisho kwa lengo la kufikisha ujumbe wa kuwashawishi wananchi kupiga kura ya maoni kubakia katika Umoja wa Ulaya, inayochukuliwa kama hatua itakaoubadilisha mustakabali mzima wa Ulaya, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amesema hakuna mtu anayejua kile kitakachotokea.

Cameron ameliambia gazeti la Financial Times kwamba hawezi kubashiri matokeo yatakuwa ya aina gani. Amesema matokeo ya kura hiyo yanaweza kwenda upande wowote kwa sababu mchuano ni mkali, ingawa amewatolea wito Waingereza wakubali kubakia katika Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: Getty Images/Sky News/Pool/C. Lobina

''Waingereza hawajiondoi. Tunajihusisha, tunaongoza, tunaleta mabadiliko, tunafanya mambo. Kama tukiondoka, majirani zetu wataendelea na mikutano na kufanya maamuzi ambayo yatatuathiri, yataiathiri nchi yetu, yataathiri kazi zetu, lakini hatutakuwepo. Watakuwa wanafanya maamuzi kuhusu sisi, bila ya sisi wenyewe kuwepo,'' amesema Cameron.

Katika jitihada za kuwashawishi wapiga kura ambao bado hawajafanya maamuzi kuhusu kura hiyo ya maoni, waendesha kampeni watazungumza katika mikutano yao ya mwisho ya hadhara. Baadae wawakilishi kutoka pande hizo mbili watakuwa na mdahalo wa mwisho wa televisheni kupitia Channel 4, utakaowashirikisha Nigel Farage, anayepinga Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya na Alex Salmond anayeunga mkono Uingereza kubakia katika umoja huo.

Kampeni zalenga masuala ya kiuchumi na uhamiaji

Kampeni kuhusu Uingereza kubakia au kujiondoa katika Umoja wa Ulaya imekuwa ikizingatia masuala mawili muhimu ambayo ni uchumi na uhamiaji, huku kila upande ukimshutumu mwenzake kwa kueneza uvumi. Kampeni hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu sana na masoko ya fedha.

Mamia ya viongozi wa makampuni makubwa duniani, akiwemo bilionea Richard Branson na tajiri anayemiliki vyombo vya habari Marekani, Michael Bloomberg, wametoa onyo kupitia gazeti la The Times, wakisema kama Uingereza itajiondoa katika Umoja wa Ulaya, hatua hiyo inaweza kusababisha ''madhara makubwa ya kiuchumi''.

Utafiti wa maoni unaonyesha kuwa kambi inayotaka Uingereza ibakie kwenye Umoja wa Ulaya inaweza kuongoza kwa ushindi mwembamba wa asilimia 51 ikilinganishwa na asilimia 49 za kambi inayotaka kujiondoa. Kura hiyo itapigwa kesho Alhamisi.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude JunckerPicha: Reuters/S. Karpukhin

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker ameionya Uingereza kwamba kupiga kura ya kujiondoa kwenye umoja huo, kunaweza kuleta madhara kwa nchi hiyo ambayo pia yatahatarisha kila kitu ambacho kimefikiwa kwa pamoja na watu wa Ulaya.

Junker ambaye anatetea umuhimu wa Uingereza kubakia kwenye Umoja wa Ulaya, amesema nchi hiyo inaweza ''ikajidhuru yenyewe'' kwa sababu kujiondoa ni kinyume na yote ambayo umoja huo na Uingereza wanayapigania.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP
Mhariri: Mohammed Khelef