kazi kubwa yamsubiri Rouhani Iran
17 Juni 2013Kwa mujibu wa baraza la ushauri nchini Iran karibu asilimia 99 ya wagombea wa uchaguzi waliondolewa na kuacha nafasi finyu ya kuweza kuleta mshangao, baada ya kubakia wagombea sita tu katika uchaguzi huo. Hassan Ruhani mwenye msimamo wa wastani pamoja na wagombea wengine watano wahafidhina waliingia katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania madaraka.
Hakuwapo mgombea ambaye ni maarufu miongoni mwa wahafidhina waliogombea uchaguzi huo , na Ruhani alikuwa hafahamiki sana. Kwa hiyo mtu angetarajia kuwa uchaguzi huo ungeingia katika duru ya pili, kwa kiasi kikubwa baina ya wagombea wawili wahafidhina. Na ghafla kila kitu kikaenda tofauti kabisa.
Uchaguzi wa rais nchini Iran umeamuliwa katika duru ya kwanza tu.
Zoezi la kuhesabu kura
Zoezi la kuhesabu kura lilikawia kuliko ilivyopangwa. Shauku ilikuwa inapanda kila dakika, hadi pale wizara ya mambo ya ndani nchini Iran ilipotoa rasmi matokeo ya uchaguzi huo.
Hakuna mtu aliyefikiria kuwa Ruhani angepata ushindi mkubwa na usio na shaka namna hiyo.
Hali hii iliwezekanaje basi?
Hali ya jamii nchini Iran ni mbaya kwa kweli. Ukosefu mkubwa wa ajira, ughali wa maisha unaopindukia mipaka, uchumi uliodumaa, vikwazo vikali na mengi mengine yanaonekana katika maisha ya kila siku katika nchi hiyo.
Na juu ya hayo linakuja pigo la kisiasa , ambalo lilitokana na ukandamizaji wa vuguvugu la maandamano baada ya uchaguzi wa mwaka 2009.
Hali kama hiyo ikiendelea kwa muda mrefu si rahisi kuizuwia na huzaa bila shaka hali ya kutoridhika , ambayo inaakisi matokeo ya uchaguzi huu.
Je ni kura ya maoni?
Matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Iran ni kura ya kukataa kabisa mpango wa kinuklia pamoja na sera za mambo ya kigeni ya wahafidhina na wakati huo huo pigo kwa kiongozi wa kidini Ayatollah Ali Khamenei.
Ndio sababu Hassan Ruhani katika muda wa chini ya wiki moja amekuwa mtu anayebeba matumaini ya wananchi wa nchi hiyo, katika kipindi hiki ambacho wananchi wamepoteza matumaini. Tangu siku ya kwanza anakabiliana na changamoto kubwa .
Anatakiwa kwa haraka kutafuta njia ya kuondoka kutoka katika mkwamo wa mazungumzo ya kinuklia, atafute muafaka na kubadilisha sera ambazo hazina tija na za kuchochea mambo. Ni kwa njia hiyo tu anaweza kuwa na matumaini ya kuupooza mzozo huo , ili kuweza kulegezwa vikwazo na pia kuifanya hali ya kijamii kuwa bora nchini mwake.
Kwa upande mwingine analazimika kuongoza upatanishi na jamii. Hali hiyo inawezekana tu , iwapo hatua za ukandamizaji dhidi ya jamii zitasitishwa, wafungwa wa kisiasa wataachiwa huru , hatua za kuwekwa kifungo cha nyumbani kwa mwanamageuzi Mussawi pamoja na Karoubi zitaondolewa , na mbali ya hayo uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uzuwiaji upatikanaji wa taarifa utaondolewa.
Bila shaka kwa kuchaguliwa Ruhani matarajio ni makubwa. Mbali ya kwamba tunatambua kuwa njia ya malengo hayo ni yenye mteremko mkubwa na yenye vikwazo vingi. Kwa upande mmoja kiongozi wa kidini , kuhusiana na masuala muhimu kama suala la kinuklia , ana usemi mkubwa. Kwa upande mwingine wahafidhina katika bunge wana nguvu kubwa.
Kwa hiyo ushindi katika uchaguzi wa rais ni hatua ya kwanza. Matumaini makubwa yanaweza kuelekeza katika kuvunjwa moyo kukubwa, watu wa Iran hilo wamekwisha kuliona mara kwa mara. Lakini mara hii, wakati ni mfupi mno na gharama za kuvunjika tena moyo ziko juu mno.
Mwandishi: Jamsheed Faroughi / ZR /Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo