1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaKenya

Kenya: Mafuriko yasababisha hali mbaya ya kiutu Dadaab

Wakio Mbogo22 Novemba 2023

Hali ya mgogoro wa ki-utu inatishia kambi ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa Kenya kufuatia mvua kubwa zinazosababisha mafuriko. Serikali ya Kenya imekosolewa kwa kutofanya vya kutosha kuikabili hali hii.

https://p.dw.com/p/4ZINo
Hali ya hewa | Mwanaume akitembea katika maji yaliotuama kutokana na mvua katika kambi ya Dadaab
Hali ya hewa | Mwanaume akitembea katika maji yaliotuama kutokana na mvua katika kambi ya DadaabPicha: Andreas Gebert/dpa/picture-alliance

John Riaga, meneja wa mawasiliano katika shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF, ukanda wa Afrika Mashariki anasema kuna haja ya dharura kuwaokoa wakimbizi wa kambi ya Daadab ambao wametafuta hifadhi kwenye shule tano eneo hilo.

Madaraja yamekatika na barabara katika eneo hilo hazipitiki, hivyo magari ya misaada hayawezi kuwafikia waathiriwa, ili kufikisha misaada ya kiutu.

Hali kwenye kambi hiyo iliyo mwenyeji wa wakimbizi 300,000 wengi wao kutoka Somalia, inaendelea kuwa mbaya kutokana na kukosekana kwa mahitaji muhimu.

Soma pia:Bandari ya Mombasa nchini Kenya imeathiriwa na mvua kubwa zinazonyesha hivi sasa na kuvuruga utaratibu wa kusafirisha mizigo na abiria

Kulingana na shirika la madaktari Wasio na Mipaka MSF, vyoo vimefurika, hakuna maji safi ya kunywa na kuna tishio la magonjwa ya mripuko kama vile kipindupindu.

Mwanzoni mwa mwaka huu, kambi ya Daadab ilishuhudia mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu na ukambi. Kumekuwepo na juhudi za kuikabili hali, ila matukio ya haya huenda yakatokomeza juhudi hizo.

Hatua za Kenya kusaidia waathirika wa mafuriko

Kulingana na naibu Rais Rigathi Gachagua kaunti 33 zimeathiriwa na mafuriko na tayari wametoa misaada kuwasaidia waathiriwa.

Ni madai ambayo wameyakana Magavana AbdulSwamad Nasir wa Mombasa na James Orengo wa Siaya. Wamesema serikali za kaunti hazijapokea shilingi Bilioni 10, za kukabiliana na athari za mvua ya El-Nino.

Soma pia:Mafuriko nchini Somalia yasababisha maelfu kuhama makaazi yao

Takwimu za Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya zinaonyesha kuwa watu 71 wamefarikikutokana na mafuriko tangu mvua kubwa ilipoanza mapema mwezi huu, huku mamia ya maelfu ya watu wakiyahama makaazi yao.