Kenya yaipeleka satelaiti yake kwenye mzingo wa dunia
15 Aprili 2023Hayo ni kulingana na ripoti ya shirika la anga za mbali la nchini Marekani la SpaceX.
Kurushwa kwa satelaiti hiyo kulitarajiwa majira ya usiku muda wa Marekani Jumatatu wiki hii, lakini kulicheleweshwa mara kadhaa kutokana na hali mbaya ya hewa.
Satelaiti hiyo ya Kenya ilisanifiwa na kikundi cha watafiti kutoka Kenya, na inanuia kutoa data kwa kilimo na kuchunguza mabadiliko ya kimazingira nchini Kenya, hususan wakati huu nchi hiyo inapokabiliwa na ukame wa muda mrefu.
Pattern Odhiambo, mhandisi wa Shirika la Kenya la Anga za Mbali, KSA, amesema satelaiti hiyo iliyopewa jina la Taifa 1, itakuwa na faida za moja kwa moja katika sekta za utafiti na kuboresha mavuno ya kilimo.
Hadi mwaka 2022, satelaiti zipatazo 50 za mataifa ya Afrika zilikuwa zimepelekwa kwenye mzingo wa dunia, kulingana na shirika la Nigeria linalofuatilia mipango ya Afrika ya anga za mbali.