Kenya yapanga mikakati ya usalama wakati huu wa uchaguzi
2 Agosti 2022Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya mashambulizi yaliyofanywa na wahalifu katika eneo la Turkana ambapo watu 11 walipoteza maisha yao.
Matiangi ametoa hakikisho kwamba maafisa wa usalama wa kutosha watapelekwa kila pembe ya nchi kuhakikisha kwamba usalama umeimarishwa wakati wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika wiki ijayo. Matiangi amewashutumu viongozi wa kisiasa wanaoeneza porojo na madai yanayotishia usalama wa taifa.
Matiangi: Demokrasia imekuwa
''Demokrasia yetu imekuwa. Watu wanaweza kubainisha kati ya mambo ya ukweli na uongo. Makamishna wa polisi wanashirikiana na viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na viongozi wa kijamii na wa nyumba kumi kujadili amani na namna ya kudumisha uwiano kwenye kaunti zao,'' alifafanua Matiangi.
Mkutano huu na asasi za usalama kutoka kaunti 14 za Bonde la Ufa kupanga mikakati ya usalama wakati huu wa uchaguzi unafanyika siku moja baada ya wahalifu kuwavamia na kuwaua watu saba kwenye eneo la Turkana katika mapigano ya kikabila. Nyumba 35 zilichomwa moto kwenye mashambulizi hayo, na watu wawili zaidi walijeruhiwa.
Maafisa wa usalama wamefanya msako na kuthibitisha kwamba wamefanikiwa kuwauwa wahalifu wanne na kuwakamata wengine. Kamishna wa Bonde la Ufa Maalim Mohammed amelaani hali ya watoto kutumika kwenye mapigano haya.
Watoto wahusishwa katika uhalifu
''Na baadhi yao walikuwa watoto wenye umri mdogo wa miaka 11 hadi 13. Sasa mtoto huyo anapata bunduki haramu kutoka wapi? Hao ni wazazi wao wanaowapa silaha, wanawaagiza kufanya wizi na mauaji na walete nyumbani. Tumewakamata wazazi hao, tunawahoji zaidi, tukiwaonya kwamba wanapaswa kuwapeleka watoto wao shuleni. Serikali imetoa elimu ya umma ya bure, kwa hiyo kwa nini umnyime mtoto haki ya kufuata ndoto yake?'' Aliuliza Mohammed.
Kampeni za uchaguzi zashika kasi Kenya
Kadhalika, Waziri Matiangi amepuuzilia mbali madai kwamba machifu na maafisa wengine wa usalama wanatumiwa na serikali kumpigia debe mgombea wa urais kupitia muungano wa Azimio Raila Odinga. Amesema taifa hili limewekwa imara na serikali kuu kupitia machifu ambao wanajitolea sana kuhakikisha amani imedumishwa na kamwe hawatosita kufanya kazi nao. Mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais, Wiliam Ruto umekuwa ukieneza madai haya kwenye kampeni zake.