Wimbi la ghasia kati ya waisrael na wapalestina lazidi
19 Oktoba 2015Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amethibitisha kuwa katika kipindi cha siku chache zijazo atakutana na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahamud Abbas kujadili namna ya kukomesha ghasia ambazo zimedumu kwa zaidi ya wiki mbili sasa na kusababisha vifo vya kiasi ya watu 41.
Kerry amezihimza pande zote mbili kujizuia kufanya vurugu kwa kuepusha vitendo vitakavyochochea ghasia zaidi na kuhakikisha hali ya utulivu imerejeshwa. Kerry anatarajiwa kukutana na Netanyahu mapema wiki hii mjini Berlin, Ujerumani na mwishoni mwa wiki anatazamiwa kukutana na Rais Abbas nchini Jordan.
Juhudi za kidiplomasia zaongezwa
Vile vile, amewataka viongozi wa pande hizo mbili kufafanua bayana suala la eneo takatifu mjini Jersalem uliopo msikiti wa Al Aqsa eneo linaloenziwa na waislamu na wayahudi na ni mojawapo ya masuala yanayozua uhasama kati ya pande hizo.
Juhudi za kidiplomasia zinakuja wakati polisi ya Israel ikithibitisha kuwa mwanamume mmoja raia wa Eritrea amefariki dunia baada ya kupigwa risasi kimakosa na kupigwa na umma katika mji wa Beersheba.
Shambulizi hilo lililotokea hapo jana usiku katika kituo cha basi katika mji huo wa kusini mwa Israel wakati mshambuliaji aliyekuwa amejihami kwa bastola na kisu alipomuua mwanajeshi wa Israel na kuwajeruhi watu wengine kumi wakiwemo maafisa wanne wa usalama.
Mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel ambao pia walimpiga risasi mwanamume huyo wa Eritrea aliyekuwa amesimama karibu na eneo hilo wakidhani ni mshambuliaji mwingine.
Wimbi hilo la ghasia kati ya waisrael na wapalestina ambalo limekuwepo kwa zaidi ya wiki mbili linazua hofu kuwa huenda kukawa na maasi makubwa kutoka kwa wapalestina huku baadhi ya wanasiasa wa Israel wakiwahimiza raia wao kuchukua silaha ili kujihami dhidi ya mashambulizi.
Usalama umeimarishwa maradufu
Israel imeimarisha usalama maradufu katika miji yake kadhaa na kutuma maelfu ya polisi wanaopigwa jeki na wanajeshi kushika doria na kulinda amani kufuatia msururu huo wa mashambulizi ya kudungwa visu hasa na vijana wa kipalestina.
Vituo vya ukaguzi vimewekwa katika maeneo ya wapalestina mashariki mwa Jerusalem ambako wengi wa washambuliaji wametokea na wanajeshi 300 wa Israel wanashika doria katika eneo hilo.
Polisi wa Israel pia wameanza kuezeka ukuta kati ya kijiji cha wapalestina cha Jabel Mukaber na mtaa wa wayahudi wa Armon Hanatziv. Huku maaafisa wa mji wa Tel Aviv wakiwazuia wafanyakazi wa kusafisha mashule kutosafisha wakati wanafunzi wako shuleni kuepusha mashambulizi.
Israel pia hapo jana ilifunga kivuko pekee kinachotumika na raia kutoka Gaza kuingia Israel na kutangaza kuwa itaruhusu tu kuingia kwa mahitaji ya kibinadamu.
Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/ap
Mhariri: Yusuf Saumu