Kiongozi wa kijeshi nchini Gabon asema hatakimbilia uchaguzi
2 Septemba 2023Katika hotuba kupitia televisheni Ijumaa (1.09.2023) Nguema amesema kuwa uongozi wa kijeshi utaendelea kuchukuwa hatua za haraka lakini kwa umakini kuepeuka chaguzi zinazorudia makosa kwa kuwarudisha madarakani viongozi walioko kwa sasa.
Muungano wa vyama vya upinzani wataka utawala wa kiraia
Haya yanajiri wakati muungano wa vyama vya upinzani wa Gabon, umetoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuhimiza viongozi waliompindua Rais Bongo, kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Msemaji wa muungano huo unaojulikana kama Alternance 2023, Alexandra Pangha, amelieleza shirika la habari la BBC kwamba wamefurahia kupinduliwa kwa Bongo, lakini wana matumaini kwamba viongozi wa mapinduzi watakabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia.
Soma pia:Gabon yasimamishwa uanachama katika Umoja wa Afrika
Muungano huo unashinikiza kuhesabiwa upya kwa kura za uchaguzi wa Jumanne, ukikariri ushindi wa mgombea wa upinzani Albert Ondo Ossa.
Nguema asema taasisi za Gabon zitazingatia zaidi demokrasia
Wakati huohuo, Nguema amesema kuwa taasisi za nchi hiyo zitazingatia demokrasia zaidi. Katika hotuba, Nguema amesema kuwa agizo la Jumatano la kuvunjwa kwa taasisi hizo ni la muda na kwamba ni suala la kuzipanga upya ili kuzifanya kuwa za kidemokrasia zaidi.
Soma pia:Viongozi wa Afrika kujibu hatua ya mapinduzi ya kijeshi Gabon
Nguema pia ameimarisha mawasiliano na makundi ya kitaifa na maslahi ya kigeni, na kukutana na wanachama wa mashirika ya kiraia siku moja baada ya hotuba kwa wafanyabiashara 200, ambao aliwasomea kuhusu rushwa.