1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa RSF Dagalo akiri kuupoteza mji mkuu wa Al-Jazira

12 Januari 2025

Jeshi la Sudan limeukomboa mji wa Wad Madani kutoka kikosi cha wanamgambo wa RSF, katika ushindi wake mkubwa zaidi katika vita vya karibu miaka miwili. Mkuu wa RSF Mohamed Daglo amekiri Jumamosi kuupoteza mji huo.

https://p.dw.com/p/4p3zh
Port Sudan, Sudan 2025 | Sherehe baada ya jeshi kuikomboa Wad Madani
Raia katika mji mkuu wa muda wa Port Sudan wakisherehekea ushindi wa jeshi la Sudan dhidi ya RSF katika mji wa Wad Madani.Picha: AFP

Kiongozi wa wanamgambo wa Sudan Mohamed Hamdan Daglo amesema Jumamosi kwamba Kikosi chake RSF kimepoteza mji mkuu wa jimbo muhimu la Al-Jazira, Wad Madani, baada ya jeshi na makundi ya wanamgambo washirika kuingia mjini humo kufuatia zaidi ya mwaka mmoja wa udhibiti wa wanamgambo hao.

Maafisa wa serikali wanaounga mkono jeshi wamepongeza kurejeshwa kwa udhibiti wa mji huo, huku kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo akiapa kuurudisha mikononi mwa wanamgambo wake.

"Leo tumepoteza raundi moja, hatujapoteza vita," alisema Daglo katika hotuba ya sauti Jumamosi jioni, akiahidi "ushindi" kwa wapiganaji wake.

Soma pia:Marekani yaishutumu Urusi kwa kufadhili vita Sudan

Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023, hali iliyosababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro mkubwa zaidi wa uhamaji duniani na tangazo la baa la njaa katika sehemu za kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika.

Luteni Jenerali wa RSF wa Sudan Mohamed Hamdan Dagalo
Mkuu wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo amekiri kuupoteza mji wa Wad Madani, lakini amesema mapambano yanaendelea.Picha: Umit Bektas/REUTERS

RSF iliiteka Wad Madani mnamo Desemba mwaka huo, na kuwahamisha mamia ya maelfu ya watu waliokuwa wamekimb*ilia huko kutoka mji mkuu Khartoum, uliopo kaskazini mwa Wad Madani.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumamosi, vikosi vya jeshi "viliwapongeza" wananchi wa Sudan kwa "vikosi vyetu kuingia katika mji wa Wad Madani asubuhi hii."

Video iliyotolewa na jeshi kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha wapiganaji wakiwa upande wa magharibi wa Daraja la Hantoub kaskazini mwa mji huo, baada ya chanzo cha jeshi kuiambia AFP kwamba walikuwa "wamelivamia lango la mashariki la mji huo."

Ofisi ya msemaji wa serikali anayeshirikiana na jeshi, ambaye pia ni Waziri wa Habari na Utamaduni Khalid al-Aiser, ilisema kuwa jeshi limeukomboa mji huo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilipongeza "ushindi mkubwa uliopatikana leo", ikisema jeshi limeuteka tena mji wa Wad Madani.

Soma pia: Jumuiya ya kimataifa haielewi athari za mgogoro wa Sudan?

Hata hivyo, jeshi bado halijatangaza rasmi kudhibiti kikamilifu mji huo. Lilisema vikosi vyake vimewaachilia huru wafungwa waliokuwa wakizuiliwa na RSF mjini humo, na kwa sasa wanafanya kazi ya "kusafisha mabaki ya waasi ndani ya mji huo."

Kwa kuwa mawasiliano yamekatwa kwa miezi kadhaa, AFP haikuweza kuthibitisha hali halisi ilivyo mjini humo kwa njia huru.

Wad Madani ni mji wa kimkakati unaounganisha barabara kuu muhimu za usambazaji zinazojumuisha majimbo kadhaa, na ndiyo mji mkubwa ulio karibu zaidi na mji mkuu Khartoum.

Sudan | Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan | Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa jeshi la Sudan na kiongozi wa nchi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: AFP

Ushindi katika mkoa wa Al-Jazira utakuwa hatua kubwa zaidi kwa jeshi tangu lilipodhibiti mji pacha wa Khartoum, Omdurman, karibu mwaka mmoja uliopita.

"Jeshi na wapiganaji washirika wamesambaa katika mitaa yote ya mji huu," shahidi mmoja aliiambia AFP kutoka nyumbani kwake katikati ya Wad Madani, akiomba jina lake libaki siri kwa sababu za kiusalama.

 Wananchi washerehekea mafanikio ya Jeshi

Jeshi na Kikosi cha RSF wote wametuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita, ikiwemo kushambulia raia na kulenga maeneo ya makazi bila kujali. Hata hivyo, RSF imekuwa ikijulikana zaidi kwa mauaji ya kiholela, uporaji wa mali, unyanyasaji wa kijinsia wa kimfumo, na kuzingira miji mizima.

Marekani ilitangaza Jumanne kwamba RSF "imefanya mauaji ya kimbari" na ikaweka vikwazo dhidi ya kiongozi wake, Mohammed Hamdan Daglo.

Kamati ya upinzani ya ndani, mojawapo ya mamia ya vikundi vya kujitolea vinavyopigania demokrasia kote nchini na vinavyoratibu msaada wa mstari wa mbele, ilipongeza hatua ya jeshi kuingia Wad Madani kama mwisho wa "udhalimu" wa RSF.

Mashahidi katika miji inayodhibitiwa na jeshi kote Sudan waliripoti makundi ya watu wakimiminika barabarani kusherehekea.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Soma pia: Urusi yapinga azimio la kusitisha mapigano nchini Sudan

Mjini Omdurman, sehemu ya jiji kuu la Khartoum lililo kilomita 200 (maili 124) kaskazini mwa Wad Madani, mashahidi waliiambia AFP kuwa watu walikuwa wakiimba "jeshi moja, watu mmoja," huku wakihofia kutaja majina yao kwa sababu za usalama.

Tangu vita vilipoanza, maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya milioni 12 wamekimbia makaazi yao, huku zaidi ya milioni tatu wakivuka mipaka, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Katika miezi ya mwanzo ya vita, zaidi ya watu nusu milioni walitafuta hifadhi Al-Jazira, kabla ya shambulizi la ghafla la RSF lililowafurusha zaidi ya watu 300,000 mnamo Desemba 2023.

Wengi wao wamekuwa wakihamahama mara kwa mara tangu wakati huo, wakati wanamgambo wa RSF wakiendelea kusonga kusini zaidi.

Soma pia: Pande hasimu nchini Sudan zakubali mazungumzo ya kusaka amani

"Tunarudi nyumbani!" umati wa watu katika mji mkuu wa muda wa Port Sudan, kwenye Bahari Shamu, ulipaza sauti barabarani Jumamosi kufuatia tangazo la jeshi.

Hata hivyo, RSF bado inadhibiti sehemu kubwa ya jimbo la Al-Jazira na karibu maeneo yote ya Darfur magharibi mwa Sudan pamoja na sehemu za kusini mwa nchi hiyo.
Jeshi linadhibiti kaskazini, mashariki, pamoja na sehemu za mji mkuu.

Chanzo: AFP