Kipi kinafuata Afghanistan baada ya Taliban kuibuka tena?
13 Agosti 2021Wakati Taliban ikidhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya miji na vijiji nchini humo, huku vikosi vya serikali ya Afghanistan vikionekana kulemewa pakubwa, haya hapa ni baadhi ya maswali na majibu yanayoweza kuelezea hali hiyo:
Taliban hawajawahi kumumunya maneno katika kuelezea kile wanachokitaka -- ambacho ni kufufua kikamilifu emara yao ya Kiislamu iliyotawala kuanzia 1996 hadi 2001. Uchambuzi mwingi na uchanganuzi vimeelekezwa juu ya namna watakavyoweza kufikia lengo lao hilo -- kupitia mazungumzo, nguvu ya kijeshi au mchanganyiko wa vyote viwili.
Soma pia:Taliban wazidi kufagia miji Afghanistan, dunia yashtushwa
Mwishowe, mkakati wa kijeshi ulidhihirisha ufanisi: vishinde kabisaa vikosi vya serikali kupitia mashambulizi ya kuratibu kote nchini. Ili kufanya hilo, walitaka kuhakikisha kwanza kwamba Marekani inaondoka nchini humo -- jambo walilofanikisha kupitia maafikiano na Washington na kuahidi kutoyashambulia maeneo ya Marekani kwa kukubali kuondoa wanaajeshi wake.
Sehemu ya muafaka huo pia ilimaanisha Washington kuishinikiza serikali ya Afghanistan kuwaachia maelfu ya wafungwa wa Taliban -- ambao wengi wao walijiunga tena na mapambano. Kwa mafanikio hayo ya kuvutia katika muda wa siku tisa, Taliban hivi sasa wamejiweka katika nafasi ya kutoa fursa kwa serikali ya kusalimu pasina masharti yoyote. Ikiwa Kabul itasita, tarajia kwamba Taliban itasonga mbele kuelekea mji mkuu kwa nguvu.
Soma pia: Taliban waichukuwa Kandahar, Marekani na Uingereza zahamisha raia
Hakuna shaka kwamba vitabu vitachapishwa na masomo kutolewa kwa miaka kadhaa kama siyo miongo kuhusu mada hii -- nini hasa kilikwenda mrama kwa vikosi usalama vya Afghanistan? Rushwa, ukosefu wa nia ya kupigana, na ombwe lililosababishwa na kujitoa kwa Marekani yumkini vyote vilitoa mchango juu ya mporomoko wa mwisho wa jeshi la Afghanistan.
Kwa miaka kadhaa, serikali ya Marekani ilitoa ripoti zinazoainisha ufisadi mkubwa ndani ya vikosi vya usalama vya Afghanistan. Makamanda walijichukulia mara kwa mara fedha zilizokususdiwa kutolewa kwa wanajeshi wao, wakauza silaha kwenye soko la magendo, na kudanganya kuhusu idadi ya wanajeshi waliomo kwenye vitengo vyao.
Taliban yajiweka katika nafasi imara ya maamuzi
Vikosi vya Afghanistan pia vilikuwa vinategemea kabisaa nguvu ya jeshi la anga la Marekani -- kuanzia kwenye lojistiki hadi mashambulizi, pamoja na usimamizi. Na kama hiyo haitoshi, vikosi vya usalama havikuwa na ujuzi wa kutosha katika masuala ya uongozi wenye ufanisi.
Soma pia: Taliban yaombwa kujiunga na serikali
Walikuwa wanasimamiwa na maafisa wa kiraia katika kasri la rais, walio na uzoefu mdogo wa kijeshi, au kupuuzwa na majenerali waliozeeka ambao walionekana kujihusisha zaidi katika mapambano madogo ya kisiasa kuliko vita kubwa zaidi iliyokuwa inawakabili. Makomando waliopewa mafunzo nchini Marekani ndiyo wlaikuwa tumaini, lakini mwisho wa siku walikuwa hawatosho kubeba jukumu la mapambano yote.
Taliban hivi ndiyo wenye sauti kubwa kila mahala. Serikali hivi sasa inadhibiti miji mikubwa mitatu tu, na haionekani kuwa na nguvu ya kuulinda kwa ufanisi mji mkuu. Watalibani wanasonga mbele kwa kasi kuelekea Kabul huku ripoti zikionesha wapiganaji wao wanapata mafanikio kwenye maeneo ya kaskazini na kusini mwa mji huo mkuu.
Marekani na jumuiya ya kimataifa yumkini wanaongeza shinikizo kwa Taliban na serikali ya Afghanistan kufikia aina fulani ya makubaliano. Lakini mwishowe, Wataliban ndiyo wako kwenye nafasi imara zaidi.
Chanzo: AFPE