1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yadai kuwakamata wageni wanaotaka kuhujumu uchaguzi

Saleh Mwanamilongo
19 Desemba 2023

Serikali ya Kongo imeelezea wasiwasi wake kuhusu tishio la kuvurugwa uchaguzi mkuu, ikidai kuwakamata raia watano wa kigeni ambao ni sehemu ya kile inachosema ni njama iliyopangwa ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/4aM3R
Uchaguzi wa Rais Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inajiandaa kwa uchaguzi wake mkuu Jumatano wiki hii, ambao unafutatiliwa kwa umakini mkubwa na jumuiya ya kimataifa.Picha: Stefan Kleinowitz/Zumapress/picture alliance

Kwenye mkutano na waandishi habari, waziri wa Kongo wa Mambo ya Ndani, Peter Kazadi Kankonde amesema kuna njama ya kuvuruga uchaguzi mkuu utakaofanyika Kongo siku ya Jumatano.

Bila kutaja majina au nchi walikotokea, Kazadi amesema watu watano ambao ni raia wa kigeni wamekamatwa. Amesema watu hao ni miongoni mwa kundi la wanaopanga njama ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo waziri wa Kongo wa mambo ya ndani Peter Kazadi amesema vikosi vya usalama vitahakikisha ulinzi wa taifa.

‘‘Ningependa kuwahakikishia jumla ya wananchi wenzetu kwamba vikosi vya usalama viko chonjo kukabiliana na kitisho cha usalama kutoka kwa maadui wa demokrasia na watu wetu. Nimethibitisha pia kwamba kesho desemba 20 uchaguzi utafanyika katika eneo zima la Kongo," alisema waziri Kazadi.

Corneille Nangaa, mkuu wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Kongo, CENI
Mkuu wa zamani wa Tume ya Uchaguzi ya Kongo, CENI, Corneille Nangaa Yobeluo, alizungumza mjini Nairobi hivi karibuni na kutishia kwamba Rais Tshisekedi hatokuwa kiongozi wa Kongo baada ya uchaguzi wa Jumatano. Picha: Luis Tato/AFP

Soma pia: Upinzani Kongo wadai kuchezewa ´rafu` kuelekea uchaguzi

Kazadi amewatolea mwito raia kubaki waangalifu na kujizuia na vitendo vya vurugu hapo kesho na wakati wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi. Serikali ya Kongo imesema haitofunga mawasiliano ya intaneti siku ya uchaguzi. Lakini haijasema ikiwa mipaka itafungwa au hapana.

Sababu za kuwakatalia waangalizi wa Umoja wa Ulaya

Akigusia sababu za kutowaruhusu waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya kuingia nchini Kongo, Peter Kazadi amesema serikali ilikuwa na wasiwasi kuhusu vifaa vya teknolojia ya kisasa vilivyoletwa na ujumbe huo wa EU ambavyo vingechangia kubadili matokeo ya uchaguzi. Lakini  waziri huyo hakutoa ufafanuzi zaidi.

Tume ya uchaguzi imerejelea msimamo wake wa kuwataka wapigaji kura kutokeza kwa wingi hapo kesho kushiriki zoezi la upigaji kura. Hata hivyo changamoto za kutawanywa kwa vifaa vya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura bado ni kitendawili katika maeneo mengi nchini.

Mtandao wa mashirika ya kiraia yanayochunguza maandalizi ya uchaguzi wa Kongo yanasema vifaa vya uchaguzi bado kuwasili kwenye maeneo mengi hasa huko Kaskazini magharibi mwa nchi. Danny Singoma, mratibu wa mtandao huo wa CERDYSOC amesema tume ya uchaguzi haijaheshimu sheria ya uchaguzi.

Rais wa DR Kongo Felix Tshisekedi
Rais Felix Tshisekedi, anawania muhula wa pili katika uchaguzi wa Jumatano.Picha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

‘‘ Kwa ujumla zoezi la kutawanya vifaa vya uchaguzi limefanyika vizuri katika miji mikubwa, lakini changamoto kubwa ni maeneo yasiofikika kwa urahisi ya nchi ambayo ni mengi. Vifaa bado kuwasili huko na ni kinyume cha sheria ya uchaguzi mabayo inataka vifaa vya uchaguzi vinatakiwa kutawanywa katika kila kituo masaa 48 kabla ya uchaguzi.‘‘

Soma pia: Uchochezi wa vita, ukabila vyatawala kwenye kampeni Kongo

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umelaani  vikali hotuba za unyanyapaa na vurugu zilizoashiria kampeni za uchaguzi nchini hapa. Umoja wa Ulaya umesema Juhudi za kugawanya watu kwa misingi ya kabila au asili yao na maoni yoyote yanayochochea vurugu hazikubaliki.