Korea Kaskazini yafyatua makombora mengine
31 Julai 2019Makombora hayo mawili yamefyatuliwa kutoka eneo la Wonsan katika pwani yake ya mashariki, na kuruka karibu umbali wa kilometa 250 hadi baharini, amesema mkuu wa utumishi wa Korea Kusini. Korea Kaskazini imepigwa marufuku kurusha makombora ya masafa mafupi chini ya maazimio ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lakini hiyo ilikuwa ni mara ya pili chini ya wiki moja, licha yamazungumzo baina ya kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un na rais Donald Trump wa Marekani.
Mfululizo wa majaribio ya makombora unaibua wasiwasi juu ya mustakabali wa mazungumzo ya wanadiplomasia wa nchi zote mbili walio na matumaini ya kuanzisha tena mazungumzo yanayolenga kuishawishi Pyongyang kuachana na shughuli za silaha za nyuklia na mpango wa makombora.
Pyongyang imeonya kuwa majadiliano hayo yatakwamishwa na hatua ya Marekani na Korea Kusini ya kukataa kufutilia mbali luteka za kila mwaka za kijeshi baina ya vikosi vyake. Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Kang Kyung amewaeleza waandishi wa habari mjini seoul kabla ya kuelekea mkutano wa nchi za Jumuiya ya Asia Mashariki ASEAN unaofanyika Thailand kuwa, "hatua ya Korea Kaskazini haisaidii kutuliza mvutano wa kijeshi na wala haisaidii kupisha njia ya mazungumzo ambayo yamepangwa".
Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo pamoja na mpatanishi wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini pia walikuwa wakielekea katika mkutano wa ASEAN, ambako Pompeo alikuwa na matumaini ya maafisa wa Marekani watakutana na wenzao wa Korea Kaskazini. Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema hapakuwa na athari yoyote ya makombora ya leo.
"Tumethibitisha kwamba hapakuwa na athari katika usalama wetu wa taifa. Tunaendelea kushirikiana kwa karibu na Marekani na wengine", alisema Abe.
Wataalamu wanasema makombora hayo ya KN-23 yametengenezwa ili kuukwepa mfumo wa ulinzi wa makombora na inakuwa rahisi kujificha na kufyatuliwa. Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong aliyaelezea makombora hayo ya KN-23 ambayo pia yalitumika katika majaribio ya wiki iliyopita kuwa ni vigumu kuzuilika. Waziri wa ulinzi wa Korea Kusini naye anakiri kwamba kuyazuia makombora ya KN-23 litakuwa jambo gumu, ingawa mfumo wake wa ulinzi wa makombora una uwezo wa kuyatambua.
Vyanzo: Reuters/AFP