1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Korea Kaskazini yaimarisha mpango wa nyuklia kwa udukuzi

10 Februari 2021

Ripoti ya ndani ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa Korea Kaskazini inaendelea na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia licha ya vikwazo vya kimataifa.

https://p.dw.com/p/3p9wb
Nordkorea Militärparade
Picha: KCNA/AP/picture alliance

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kamati ya usimamizi wa vikwazo dhidi ya taifa hilo, inasema serikali mjini Pyongyang imeuendeleza mpango wake wa nyuklia na makombora ya masafa marefu, katika ukiukaji wa maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Licha ya kwamba mwaka 2020 hakuna majaribio ya silaha za nyuklia au makombora yaliyosajiliwa, Korea Kaskazini iliendelea bado kutengeneza vifaa vya nyuklia, kuendeleza vituo vyake vya nyuklia na kuboresha miundombinu ya makombora ya masafa marefu.

Ripoti hiyo iliyotumwa kwa wanachama wa Baraza la usalama siku ya Jumatatu, inasema kuwa wizi jumla wa mali za mtandaoni wa Korea Kaskazini kuanzia 2019 hadi Novemba 2020 unakadiriwa kuwa na thamani ya karibu dola milioni 316.4, kwa mujibu wa nchi moja ambayo haikutajwa jina.

Soma pia: Korea Kaskazini: Hatuna mpango wa mazungumzo na Marekani

Kamati hiyo ilisema uchuguzi wake uligundua kuwa watendaji wanaohusishwa na Korea Kaskazini walifanya operesheni mwaka 2020 dhidi ya taasisi za kifedha na majumba ya kubadilisha fedha za kimtandao, na kuingiza fedha za kusaidia programu zake za silaha za maangamizi makubwa.

Nordkorea Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.Picha: KCNA/REUTERS

Katika uendelezaji wa mpango wake wa silaha, watalaamu wanasema serikali ya Kim Jong Un pia imetengeneza nyenzo za kuendeleza mnyororo wa mgawanyo wa nguvu za atomu, ambao ni kiambata muhimu katika utengenezaji wa silaha za nyuklia, na pia kudumisha miundombinu yake ya nyuklia.

Wataalamu hao wamesema Korea Kaskazini ilionyesha mifumo ya makombora ya masafa mafupi, ya kati, na marefu wakati wa magwaride ya kijeshi. Pia ilitangaza maandalizi ya jaribio na utengenezaji wa silaha mpya, na iliimarisha miundombinu ya makombora yake ya masafa marefu.

Uwezo wa kukwepa vikwazo

Kamati hiyo ilipendekeza kwamba Baraza la Usalama liwawekee vikwazo wanaume wanne wa Korea Kaskazini, ambao ni Choe Song Chol, Im Song Sun, Pak Hwa Song na Hwang Kil Su.

Korea Kaskazini yafyatua tena makombora

Baraza la usalama limeiwekea vikwazo Korea Kaskazini tangu ilipofanya jaribio lake la kwanza ya kifaa cha nyuklia mwaka 2006. Limepiga marufuku sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya bidhaa zake na kupunguza manunuzi, likijaribu kuishinikiza Pyongyang kuachana na mipango yake ya nyuklia na makombora.

Soma pia: Korea kusini yaonesha hofu ya silaha za Korea kaskazini

Lakini muhtasari wa ripoti hiyo na baadhi ya ugunduzi wake na mapendekezo, vinabainisha wazi kwamba Korea Kaskazini bado ina uwezo wa kukwepa vikwazo na kuendeleza silaha zake na pia kuingiza kinyume cha sheria mafuta yaliyosafishwa ya petroli, kupata huduma za kimataifa za kibenki na kuendesha shughuli ovu za mtandaoni.

Agosti 2019, Kamati hiyo ya wataalam wa Umoja wa Mataifa ilisema wataalam wa mtandao wa Korea Kaskazini walipata kwa njia haramu, kiasi kinachokadiriwa kufikia dola bilioni 2 kufadhili mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.

Kamati hiyo imesema katika ripoti mpya kwamba ilichunguza shughuli ovu zinazofanywa na ofisi kuu ya upelelezi, ambayo imo kwenye orodha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, zikiwemo kulenga mali za mtandaoni na watoa huduma za mali mtandaoni, na mashambulizi dhidi ya kampuni za ulinzi.

Nordkorea stellt neue Rakete bei Militärparade vor
Korea Kaskazini inaamini kuimarisha shehena yake ya silaha za nyuklia na makombora ni kinga dhidi ya mashambulizi yanayoweza kufanywa dhidi yake na Marekani.Picha: KCNA/Reuters

Kamati hiyo imesema inachunguza udukuzi wa Septemba 2020 dhidi ya kampuni ya biashara ya sarafu ya mtandaoni ambao ulipelekea wizi wa sarafu za mtandaoni zenye thamani ya karibu dola milioni 281, ambazo uchunguzi unaonyesha zinahusishwa na udukuzi wa pili wa dola milioni 23 uliofanyika Oktoba 2020.

Kwa mujibu wa nchi moja ambayo haikutajwa, Korea Kaskazini pia inaendelea kuingiza mapato haramu kupitia majukwaa huru ya tehama, ikitumia mbinu sawa na zile inazotumia kuifikia mifumo ya fedha ya kimataifa - ambazo ni utambulisho wa bandia, matumizi ya huduma za mitandao ya siri ya mawasiliano, na kuanzisha kampuni za siri jimboni Hong Kong.

Chanzo: Mashirika