Korea Kaskazini yarusha makombora mengine ya masafa ya mbali
9 Oktoba 2022Maafisa wa Korea Kusini walisema kasi hii ya majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini inaashiria kuwa Pyongayang ipo karibuni zaiid kurejea majaribio ya silaha zake ya nyuklia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017.
Makombora yote mawili yaliyorushwa Jumapili (Oktoba 9) yalitua umbali wa kilomita 100 na kujichawanya umbali wa kilomita 350, kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Japan, Toshiro Ino.
Kombora la kwanza lilirushwa majira ya saa 7:47 usiku na la pili likarushwa dakika sita baadaye, ambapo yote mawili yalituwa nje ya eneo huru la kiuchumi la Japan.
"Tunachunguza ni aina gani ya makombora na endapo yalikuwa makombora ya masafa ya mbali yanayoweza kurushwa kutokea nyambizi baharani," alisema Waziri Toshiro.
Marekani haijaona kitisho cha moja kwa moja
Jeshi la Marekani lilisema linafanya mashauriano na washirika wake, Korea Kusini na Japan, na washirika wengine wa kimataifa kufuatia makombora hayo, ambayo ilisema yanaonesha "nguvu za kuharibu" za programu ya makombora na silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini.
"Majaribio hayo ya karibuni kabisa kutoka eneo la Mucheon katika pwani ya mashariki mwa Korea Kaskazini ni uchokozi mkubwa ambao unaidhuru amani," zilisema mamlaka za Korea Kusini.
Hata hivyo, Kamandi ya Jeshi la Marekani katika Indo-Pasifiki ilisema kwenye tathamini yake kwamba ufyatuaji huo wa makombora bado haujawa kitisho kwa Wamarekani waka washirika wao.
"Ahadi ya Marekani katika kuzilinda Jamhuri ya Korea (Kusini) na Japan ipo pale pale," ilisema Kamandi hiyo kwenye taarifa yake.
Siku ya Jumanne (Oktoba 4) Korea Kaskazini ilifanyajaribio la komborala masafa marefu zaidi kuliko ilivyowahi kufanya kabla, ambalo liliruka kupindukia Japan kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitano na kusababisha onyo litolewe kwa wananchi kusaka maeneo ya kujificha.
Ino alisema Tokyo isingelivumia matendo hayo ya kila mara ya Korea Kaskazini. Ilikuwa ni mara ya saba kufanyika majaribio kama hayo tangu tarehe 25 Septemba.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Japan ilisema wajumbe wake wa masuala ya nyuklia walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na wenzao wa Korea Kusini na Japan, ambapo walikubaliana kwamba majaribio ya makombora ya masafa marefu ya Korea Kaskazini yanatishia amani na usalama wa eneo hilo na pia jumuiya ya kimataifa, sambamba na kutishia usalama wa usafiri wa anga.
Korea Kaskazini yasema inajilinda
Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikifanya majaribio ya makombora na nyuklia licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ilisema siku ya Jumamosi (Oktoba 8) kwamba majaribio hayo yalikuwa ni kwa ajili ya kujilinda dhidi ya vitisho vya moja kwa moja vya jeshi la Marekani na havijadhuru usalama wa majirani zake.
"Majribio yetu ya makombora ni ya hatua ya kawaida ya kuulinda usalama wa nchi yetu na amani ya eneo hili kutokana na vitisho vya kijeshi vya Marekani," iliseme taarifa ya shirika la habari la nchi hiyo (KCNA) ikimnukuu msemaji wa idara ya anga.
Korea Kusini na Marekani zilifanya mazoezi ya pamoja ya jeshi la baharini siku ya Ijumaa, siku moja tu baada ya Korea Kusini kutuma ndege zake za kijeshi kujibu mazoezi ya kijeshi ya Korea Kaskazini.
Marekani pia ilitangaza vikwazo vipya siku hiyo kujibu majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini.
Jirani wa Korea Kaskazini, China, iliyanyooshea kidole mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na washirika wake katika Rasi ya Korea ilipoulizwa juu ya majaribio ya siku ya Jumapili.
"Maneno ya Marekani yanapaswa kuwiana na matendo yake, msimamo wake ambao hauna dhamira mbaya kuelekea Korea Kaskazini lazima utafsirike kivitendo, inapaswa kuunda mazingira ya kurejea kwenye majadiliano yenye maana," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni, Mao Ning.