Kramp-Karrenbauer kuapishwa waziri mpya wa Ulinzi Ujerumani
24 Julai 2019Kramp-Karrenbauer, ambaye mwaka uliopita alimpokea Kansela Angela Merkel wadhifa kama kiongozi wa chama cha Christian Democratic Union, (CDU), sasa anachukua pia wadhifa wa waziri wa Ulinzi uliokuwa wa Ursula von der Leyen ambaye amechaguliwa mapema mwezi huu kuwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.
Waziri huyo mpya wa ulinzi anajitahidi kuvivutia vikosi vya ulinzi upande wake ili vimkubali. Kramp-Karrenbauer amesisitiza kwamba Ujerumani inavihitaji vikosi hivyo. Na kuwahakikishia kwamba naye yuko kwa ajili yao.
"Lakini nasema waziwazi: asante peke yake haitoshi. Huduma yenu inahitaji heshima, shukrani na msaada. Ninajua Ujerumani inaweza kukutegemeeni, na ninakuambieni: munaweza nanyi kunitegemea," amesema Kramp-Karrenbauer.
Matamshi hayo aliyasema mjini Berlin, mnamo Julai 20, akiwa katika hafla ya kuadhimisha miaka 75 tangu mpango maarufu ulioshindikana wa kumuua Adolf Hitler.
Kiongozi mwenye majukumu mawili
Lakini itachukua muda hadi Kramp-Karrenbauer, aweze kuaminiwa na wanajeshi wa Ujerumani. Nariman Hammouti-Reinke, mjumbe wa jeshi la majini la Ujerumani ameiambia DW kwamba haitokuwa kazi rahisi kwa waziri huyo.
Hammouti-Reinke anaeishi karibu na mji wa Bremen, anaongoza chama cha Deutscher.Soldat, ambacho kinalenga kuongeza idadi ya watu wa makabila tofauti ndani ya jeshi la Ujerumani. Ameonya kwamba wanajeshi ni watu wanaokasirika mara moja, kwahiyo waziri huyo mpya atalazimika kuchagua maneno yake kwa uangalifu.
Ameongeza kwamba jeshi hilo la Ujerumani Bundeswehr limeshasikitishwa sana na mawaziri wa zamani wa ulinzi. Waziri aliyemtangulia Kramp-Karrenbauer, ambaye ni Ursula von der Leyen, mnamo mwaka 2017 alililaumu jeshi kwa kushindwa kukabiliana na wanajeshi wenye misimamo mikali ya siasa za mrengo wa kulia waliomo ndani ya jeshi hilo.
Kutokana na hilo, Kramp-Karrenbauer alihakikisha anajiweka mbali na matamshi hayo ya von der Leyen. Katika gazeti la kila Jumapili la Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung, aliweka wazi kwamba sio kila mwanajeshi anaeshukiwa kwa madai hayo.
Jürgen Görlich, naibu mkuu wa BundeswehrVerband, chama kinachowakilisha wanajeshi, anaamini kuwa na majukumu mawili kwa wakati mmoja kunaweza kulisaidia jeshi. Ameeleza kwamba sasa jeshi limepata kiongozi mwenye ushawishi wa kisiasa. Kitu ambacho hakikuwahi hutokea tangu miaka ya 1960, wakati Frank-Josef Strauss alipohudumu kama waziri wa ulinzi pamoja na kiongzi wa hama cha Christian Social Union, chama ndugu kwa CSU cha jimbo la Bavaria.
Soma zaidi:Mfahamu Annegret Kramp-Karrenbauer, kiongozi mpya wa CDU
Chanzo: (dpa,dw)