Lavrov awasili Syria
7 Februari 2012Serikali hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa la kutakiwa ijiuzulu kutoka kwa waandamanaji kwa zaidi ya miezi 11 sasa, imedai inakabiliana na makundi ya kigaidi yenye silaha katika mji huo. Hatua hiyo inatakelezwa katika mji huo ambao unajulikana kama kiini cha vuguvugu la maandamano, kutokea vurugu zilizosababisha vifo vya kiasi ya watu kadhaa kwa siku nne mfulululizo.
Mfululizo wa mashambulizi haya ya sasa unfanyikia wakati ambapo anawasili Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, pamoja na Mkuu wa Usalama wa Nje, Michael Fradkov.
Mpaka sasa ripoti zinaeleza kuwa maafisa hao wa ngazi ya juu ya Urusi wana nia ya kufanikisha jitihada za kumfanya Rais Assad ajiuzulu.
Katika maeneo ya Homs, milio ya risasi imesikika mapema asubuhi katika maeneo yaliokuwa yakidhibitiwa na waasi wa wilaya ya Baba Amro. Milio hiyo ilijibiwa na mashambulio makubwa ya mizinga na maroketi katika ngome yao hiyo.
Mmoja kati ya wanaharakati, Abu Rami, aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kwa njia ya simu, akiwa mjini Beirut, kwamba miripuko hiyo ilisikia usiku wote wa kuamkia leo.
Alisema kumekuwa na hali mbaya sana katika eneo hilo, hakuna mtu anaeweza kutoka nje hata kidogo, kumekuwa na wadunguaji wa risasi kila mahala.
Wanaharakati wengine wanasema katika eneo hilo kumekuwa na upungufu mkubwa wa vyakula na madawa. Wameongeza kuwa mashambulizi hayo yanatokea siku moja baada ya kuuwawa kwa zaidi ya watu 100 katika vurugu zilizotokea katika maeneo tofati ya Syria.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria limesema kiasi cha raia 69 waliuwawa jana pekee katika mji wa Homs, huku idadi nyingine ya watu 13 wakiuwawa huko katika jimbo la kaskazini magharibi la Idlib, mmoja Aleppo, na wengine karibu 15 karibu kabisa na jiji la Damascus.
Kwa ujumla makundi ya haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 6,000 wameuwawa tangu kuanza kwa vuguvugu la mageuzi katikati ya Machi mwaka jana.
Katika mkanda wa video uliosambazwa kupitia mtandao wa YouTube umeonesha hospitali moja imeshambuliwa kwa makombora ya mizinga, huko Baba Amro na wagonjwa wamelala katika machera ardhini, huku wakizingwa na dimbwi kubwa la damu
Safari ya Lavrov nchini Syria inafanyika siku chache baada ya kushindwa juhudi za kuutatatua mgogoro huo kwa njia za kidiplomasia baada ya Urusi na China kupiga kura ya turufu ya kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lililengwa dhidi ya serikali ya Syria, mshirika huyo wa Urusi tangu zama za Vita Baridi.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Miraji Othman