1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yafanyika kupinga chama cha siasa kali cha AfD

26 Februari 2024

Maelfu ya watu wameingia katika mitaa ya miji mbalimbali ya Ujerumani kuandamana kukipinga chama cha siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/4csD2
Berlin 2024 | Waandamanaji wamekusanyika katika bunge la Ujerumani kupinga siasa kali za mrengo wa kulia
Waandamanaji wamekusanyika katika bunge la Ujerumani kupinga siasa kali za mrengo wa kuliaPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Waandamanaji walikusanyika chini ya kauli mbiu, "Sisi ndio Kinga," kauli inayotumika kupinga uungwaji mkono wa siasa za mrengo wa kulia nchini Ujerumani tangu vita vya pili vya dunia.

Maandamano makubwa yalifanyika katika mji wa kaskazini wa Hamburg, ambako takriban watu 50,000 walikusanyika. Hamburg ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani.

Waandamanaji waliimba nyimbo za "Hatutaki Wanazi, Hatutaki AfD," wakimaanisha Alternative für Deutschland yaani chama mbadala kwa Ujerumani kisichopenda wageni.

Waandaji wa maandamano hayo wametoa wito kwa watu kusimama kidete kutetea demokrasia.

Hivi karibuni, Ujerumani imeshuhudia wimbi la maandamano dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia baada ya ripoti kufichua kuwa maafisa wa AfD walikuwa na mkutano na kundi la watu wanaopigania sera za kuwafukuza watu wote wasiokuwa na asili ya Ujerumani.