1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aanza ziara nchini Marekani

30 Novemba 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajia kukutana na rais Joe Biden baadae leo, anapoanza ziara yake nchini Marekani ambayo pamoja na mengineyo inalenga kuangazia mahusiano ya kimkakati baina ya mataifa hayo.

https://p.dw.com/p/4KHSb
 Emmanuel Macron
Picha: Thibault Camus/AP/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anazuru Marekani wakati pia kukiwa na wasiwasi katika suala zima la ushirikiano wa kibiashara kati ya Ulaya na Marekani. 

Macron akiongozana na mkewe Brigitte na maafisa wengine wa ngazi za juu wamewasili jana usiku nchini Marekani tayari kwa ziara hiyo ya siku mbili, itakayomalizika siku ya Ijumaa kwa kuutembelea uliowahi kuwa mji wa Ufaransa wa New Orleans huko Louisiana.

Hii ni ziara ya kwanza rasmi kufanywa na Macron katika ikulu ya White House chini ya utawala wa rais Joe Biden, baada ya hapo kabla kuvurugwa na vizuizi vya UVIKO-19. Maafisa wa Marekani wamesema hatua ya Ufaransa ya kuzuru taifa hilo inaakisi mahusiano yao ya kihistoria, lakini pia jukumu muhimu lililobebwa na Paris ndani ya Umoja wa Ulaya, na hasa katika kuikabili Urusi iliyoivamia Ukraine.

Weltspiegel | 01.06.2021 | USA - Memorial Day
Eneo la makaburi ya kitaifa la Arlington nchini Marekani, ambalo linatembelewa pia na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Michael A. McCoy/REUTERS

Hii leo Macron anatembelea eneo la kitaifa la makaburi la Arlington, kisha atakutana na makamu wa rais Kamala Harris na kujadiliana naye kuhusu ushirikiano wa teknolojia ya angani, katika makao makuu ya shirika la anga za mbali la Marekani, NASA mjini Washington. Siku yake ya kwanza itakamilika kwa kupata chakula cha jioni , pamoja na rais Joe Biden na wake zao.

Siku ya Alhamisi ndio itakayokuwa na matukio muhimu ambayo ni pamoja na gwaride la heshima katika ikulu ya White House, mazungumzo katika ofisi ya rais, mkutano wa pamoja kati yake na Biden na waandishi wa habari na hafla ambayo mwanamuziki na mshindi wa tuzo ya Grammy Jon Batiste atatumbuiza.

Tofauti na ziara ya Macron mwaka 2018, wakati huo akiwa rais Donald Trump, ziara ya sasa itajikita zaidi katika mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa hayo. Ikumbukwe kwamba mahusiano ya kidiplomasia baina yao yaliingia dosari mwaka jana baada ya Australia kuvunja makubaliano na Ufaransa ya kununua nyambizi, na badala yake ikaingia makubaliano mapya na Marekani. Hata hivyo walimaliza tofauti zao.

USA US-Präsident Joe Biden
Mpango wa rais Joe Biden wa kuwekeza mabilioni ya dola kwenye nishati rafiki umepeleka hofu kwa mataifa ya Ulaya.Picha: Michael Reynolds/MediaPunch/IMAGO

Lakini wasiwasi ungali ukiongezeka na hasa katika eneo la kibiashara wakati Ulaya ikifuatilia kwa mashaka makubwa hatua ya Biden ya kusaini Sheria ya Kupunguza Mfumuko wa Bei ama IRA. Sheria hiyo itaruhusu kuingizwa mabilioni ya dola kwenye teknolojia rafiki za mazingira kwa kutumia bidhaa zinazotengenezwa nchini humo.

Ulaya inahofia kutokuwepo na usawa, wakati Marekani ikifaidika zaidi katika sekta hiyo, katika wakati ambapo mataifa hayo yanahangaishwa na athari za kiuchumi zilizochochewa na vita vya Ukraine na majaribio ya nchi za magharibi ya kuondoa utegemezi wa nishati ya Urusi. Changamoto nyingine ni inayolikumba bara hilo gharama kubwa za usafirishaji wa gesi ya kimiminika kutoka Marekani, ambayo pia mahitaji yake yameongezeka.

Soma Zaidi: Viongozi wa dunia wailaani Urusi kuhusu Ukraine

Hata hivyo msemaji wa masuala ya usalama wa taifa katika ikulu ya White House John Kirby amewaambia waandishi wa habari wa Ufaransa kwamba kwa sasa wako tayari kuwasikiliza washirika wao wa kibiashara.

Mashirika: AFPE