Madai ya Israel kukwamisha mazungumzo ya kusitisha mapigano
20 Agosti 2024Maafisa walio na karibu na mazungumzo hayo wanasema Israel inataka kuendeza uwepo wa kijeshi katika njia nyembamba kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri ambayo inauita ukanda wa Philadelphia, pamoja na eneo ililoliunda linaloitenganisha Gaza Kaskazini na Kusini.Je, maeneo hayo yana umuhimu gani kwa Israel?
Haijabainika wazi iwapo udhibiti wa Israel wa njia hizi umejumlishwa katika pendekezo linaloungwa mkono na Marekani ambalo waziri wa mambo wa nje Antony Blinken ameitolea wito Hamas kulikubali ili kuondoa mkwamo katika mazungumzo ya kusitisha vita.
Blinken ambaye amerejea kwenye Kanda ya Mashariki ya Kati wiki hii, alisema Jumatatu kwamba Israel ilikubaliana na pendekezo hilo bila kusema linahusisha nini hasa.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema udhibiti wa eneo la mpakani na Misri unahitajika kuzuwia uwezo wa Hamas kujaza upya ghala lake la silaha kupitia njia za magendo, na kwamba Israel inahitaji mfumo wa kuzuwia wapiganaji kurejea upande wa kaskazini, ambo umetengwa kwa kiasi kikubwa tangu Oktoba.
Soma pia:Hamas yasema Biden anaipa Israel "Tiketi" ya kundeleza vita
Hamas imayakataa madai hayo, ambayo yaliwekwa wazi katika wiki za karibuni. Hakukutajwa suala la Israel kuendeleza udhibiti wa njia hizo katika rasimu za awali na pendekezo linalobadilika la kusitisha vita ambazo shirika la Associated Press liliona nakala zake.
Hamas inasema uwepo wa kudumu wa Waisrael Gaza utakuwa sawa na ukaliaji wa kijeshi. Misri, ambayo imehudumu kama mpatanishi muhimu katika mazungumzo ya miezi kadhaa, pia inapinga vikali uwepo wa Israel katika upande wa apili wa mpaka wake na Gaza. Kwa nini njia hizo ni mhimu na kwa nini Israel inazitaka?
Njia ya Philadelphia ni ukanda mwembamba wenye upana wa karibu mita 100 na urefu wa kilomita 14 ulioko upande wa Gaza wa mpaka na Misri, ukihusisha kivuko cha Rafah, ambacho hadi kufikia mwezi Mei kilikuwa nji pakee ya Gaza kwenye ulimwengu wa nje isiyodhibitiwa na Israel.
Israel: Hamas inatumia njia hizi kuingiza silaha
Israel inasema Hamas ilitumia mtandao mpana wa njia za chini ya ardhi zilizoko chini ya mpaka huo kuingiza silaha, na kuiruhusu kujenga uwezo wa kijeshi iliyoutumia Oktoba 7 kuishambulia. Jeshi la Israel linasema limegundua na kuharibu mahandaki kadhaa tangu kuiteka njia hiyo mwezi Mei.
Misri inakanusha madai hayo, ikisemailiharibu mamia ya mahandaki kwa upande wake wa mpaka miaka mingi iliyopita na kuunda kizuwizi chake cha kijeshi dhidi ya magendo.
Ukanda wa Netzarim wenye urafu wa karibu kilomita nne unaanzia mpaka wa Israel hadi pwani kusini mwa mji wa Gaza na unautenga mji huo mkuu wa Gaza na maeneo mengi ya kaskazini na kusini.
Hamas imetaka mamia ya maelfu ya Wapalestina waliokimbia kutoka upande wa kaskazini waruhusiwe kurudi kwenye makaazi yao. Israel imaridhia takwa hilo lakini inataka kuhakikisha hawana silaha.
Udhibiti wa Israel wa njia hizo utahitaji kufungwa kwa barabara, nyuzio, minara ya walinzi na miundombinu mingine ya kijeshi, kama vile vituo vya ukaguzi wa kijeshi vinavyoshuhudiwa katika eneo linalokaliwa kimabau na Israel la Ukingo wa Magharibi, na pia Gaza katika kipindi cha kabla ya kujiondoa mwaka 2005.
Soma pia:al-Sisi atahadharisha juu kusambaa vita kwa viwango vya juu alipokutana na Blinken
Israel inasema vituo kama hivyo vya ukaguzi vinahitajika kwa ajili ya usalama, lakini Wapalestina wanavitazama kama uingiliaji wa kijeshi katika maisha yao ya kila siku.
Vinatazamwa pia na Wapalestina wengi kama kitangulizi cha ukaliaji wa kudumu wa kijeshi na kurejeshwa kwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, jambo ambao washirika wa serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Netanyahu wametaka waziwazi.
Hamas inataka uondoaji kamili wa jeshi la Israel na inamtuhumu Netanyahu kuweka masharti mapya ili kuhujumu mazungumzo.
Misri kwa upande wake, inasema operesheni za Israe kwenye mpaka zinatishia makubaliano ya kihistoria ya amani kati ya mataifa hayo mawili, na imekataa kufungua upande wa wake wa kivuko cha Rafah, hadi Israel itakaporejesha upande wa Gaza chini ya udhibiti wa Wapalestina.