Madai ya njama za kuiba kura kaunti ya Kwale
11 Agosti 2022Mchakato wa kujumlishwa kura umesimamishwa kwa muda katika kituo cha kujumlishia kura cha Matuga kaunti ya Kwale pwani ya Kenya baada ya baadhi ya wagombea akiwemo anayewania ugavana wa chama cha ODM Hamadi Boga na mgombea wa useneta Salim Mwadumbo kutoa malalamishi kuwa kuna njama ya kura kuibwa.
Viongozi hao wanalalamika kuwa mawakala wao wamekuwa wakikatazwa kuingia kwenye vituo hivyo kushuhudia matokeo yaliyopo kwenye karatasi za kura zilizohesabiwa. Na katika kaunti ya Mombasa kutangazwa kwa washindi wa viti mbalimbali kunatarajiwa kufanyika mapema leo.
Umekuwa usiku mrefu kwa maafisa wa IEBC wanaoendesha zoezi la kujumlishwa kwa kura katika kituo cha Matuga kaunti ya Kwale pwani ya Kenya.
Soma pia: Kenya: Uchaguzi wa gavana Mombasa na Kakamega waahirishwa
Baadhi ya viongozi, mmoja wao akiwa aliyewania ugavana na mrengo wa ODM Hamadi Boga wameingia kwenye kituo hicho wakilalamika kuwa kuna njama ya kura kuibwa. Inasemekana kuwa kuna baadhi ya maafisa wanaoshughulika na kujumlisha kura waliokamatwa.
Na katika kituo cha kuhesabia kura cha Babla, wananchi wamekesha usiku kucha wakisubiri kutangazwa kwa washindi wa uchaguzi huu. Wengine walikuwa wanaimba na kucheza kama njia moja ya kuhakikisha kuwa hawalali wakapitwa.
Kwengineko katika kaunti ya Mombasa baadhi ya vituo vya kujumlisha kura vinatarajiwa kuchelewesha kuwatangaza washindi wa uchaguzi. Haya yanajiri kutokana na kuchelewa kuanza kwa shughuli ya kujumlisha kura katika vituo vya nyali,changamwe na kisauni.
Wario Ibrahim Ali ni msimamzi wa kituo cha eneo la Shanzu ameeleza kuwa bado wanaendelea na zoezi hilo la kujumlisha kura kwa utulivu. Wario amepongeza kuweko kwa amani katika eneo bunge la Kisauni.
Kaunti ya Mombasa ni moja ya kaunti nchini Kenya ambapo uchaguzi wa Ugavana ulihairishwa,uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu wa Agosti.