Kenya: Uchaguzi wa gavana Mombasa na Kakamega waahirishwa
8 Agosti 2022Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imetangaza uamuzi wake jioni ya mkesha wa siku ya uchaguzi, bila kueleza chaguzi hizo zilizoahirishwa zitafanyika lini.
Uchaguzi mwingine ulioahirishwa na tume ya IEBC ni ule wa viti vya ubunge vya Kacheliba na Pokot Kusini, kwa maelezo yale yale ya taarifa kwenye karatasi kutokuwa sahihi.
Soma zaidi: Kampeni za uchaguzi zimemalizika nchini Kenya lakini taarifa potofu zaendelea mitandaoni.
Awali ilikuwa imeelezwa kuwa karatasi za kupiga kura ya ugavana wa Kilifi yalikuwa yamepelekwa katika kaunti ya Mombasa, huku ya Mombasa yakiwa hayajulikani yaliko. Licha ya hali hiyo, maafisa wa IEBC walisema tatizo hilo liko katika uwezo wao kulitatua.
Wananchi kutoka Mombasa wameeleza kukerwa na kukasirishwa na tukio la kuahirisha uchaguzi wa gavana wao.
Usambazaji wa vifaa waendelea kwingineko
Hayo yakiarifiwa, shughuli ya usambazaji wa vifaa vya kupigia kura zimeanza Jumatatu nchini Kenya. Makasha ya makaratasi, masanduku ya kutumbukiza kura na vifaa vyengine vitakayotumika siku ya uchaguzi vilikuwa vinawasilishwa kwenye vituo vya kupigia kura.
Aidha mkuu wa usalama katika eneo bunge la nyali Daniel Mumasaba amewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao na wala wasijali kuhusu usalama kwani wamejiandaa vilivyo kuhakikisha kuwa usalama umeimarika.
Soma zaidi: Kenya yapanga mikakati ya usalama wakati huu wa uchaguzi
Kaunti ya Mombasa ina wapiga kura Laki sita,elfu arobaini na moja mia tisa kumi na tatu (641,913) na kuna vituo elfu moja na arobaini na moja (1,041) vya kupigia kura katika wadi sita za Mombasa ambazo ni Changamwe, Jomvu, Kisauni, Nyali, Likoni na Mvita:
Ukame watishia uitikiaji wa wapigakura Marsabit
Kaskazini mwa Kenya, wanasiasa katika jimbo la Marsabit wanahofia kuwa huenda kukashuhudiwa idadi ndogo ya wapigakura jimboni humo kutokana na ukame unaoshuhudiwa.
Wanasiasa hao sasa wanaitaka serikali kuhakikisha wakaazi walioathirika na makali ya ukame wanapewa maji wakati huu wa shughuli ya upigaji kura.
Kulingana na Naomi Jillo, mgombea kiti cha uwakilishi wa kike katika jimbo hili, iwapo serikali haitawafikia kwa chakula au maji wakaazi walioathirika na makali ya ukame, huenda idadi kubwa ya wakaazi wasijitokeze.
Ripoti na Halima Gongo (Mombasa) na Michael Kwena (Marsabit)