1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBangladesh

Maelfu ya wabangladesh waadamana kudai haki za waliouawa

3 Agosti 2024

Maelfu ya watu wa Bangladesh wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Dhaka kudai haki kwa zaidi ya wanafunzi 200 waliouawa katika wimbi la ghasia za mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/4j57b
 Bangladesh
Mamia ya waandamanaji mjini Dhaka nchini BangladeshPicha: Sazzad Hossain/DW

Maelfu ya watu wa Bangladesh wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Dhaka kudai haki kwa zaidi ya wanafunzi 200 waliouawa katika wimbi la ghasia za mwezi uliopita katikati mwa maandamano dhidi ya mfumo wenye utata wa upendeleo wa nafasi za kazi serikalini.

Mara hii waliojitokeza kuandamana ni wanafunzi wenyewe,  madaktari, wazazi na walimu ambao wameonekana wakiwa wamebeba mabango yanayosomeka "Tunataka haki" na pia yakimshinikiza Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajiuzulu na kisha ashtakiwe. 

Mpaka sasa mamlaka nchini humo zimezifunga shule na vyuo vikuu kote Bangladesh, kufungwa kwa huduma ya mtandao pamoja na kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje.

Maandamano yanayoendelea yamekuwa changamoto kubwa kwa uongozi wa Hasina, ambaye alirejea madarakani kwa muhula wa nne mfululizo mwezi Januari mwaka huu uchaguzi uliosusiwa na wapinzani wake wakuu.