1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli awaangukia wapigakura wa Arusha kubadili njia

23 Oktoba 2020

Chama cha mapinduzi CCM kimefanya kampeni za urais mkoani Arusha kaskazini mwa Tanzania ikiwa ni kampeni za mwisho kwa eneo hilo, na kusema ana mipango mingi tu ya maendeleo kwa mkoa huo ikiwa atapewa fursa.

https://p.dw.com/p/3kMJ4
Tansania Dodoma VEröffentlichung Parteiprogramm der CCM | John Magufuli
Picha: DW/E. Boniphace

Dr. John Pombe Magufuli ambaye anatetea kiti chake cha urais katika uchaguzi huu, mara kadhaa amekuwa akisikika katika mikutano yake ya siasa akisema kuwa utofauti wa vyama vya siasa hauwezi kuzuia maendeleo kwani maendeleo hayana vyama.

Katika viwanja vya Shekh Amri Abeid jijini Arusha, Magufuli amerejerea kauli yake ya kusema maendeleo hayana vyama akimaanisha yeye kama Rais haongozwi na itikadi za vyama vya siasa kuleta maendeleo na ndio maana amefanya mambo mengi ya maendeleo katika jiji la Arusha licha ya kwamba mbunge wa Arusha mjini alikuwa wa chama cha upinzani.

Soma pia: Magufuli kuhitimisha kampeni za Dar es salaam

"Ninachotaka kuwaomba ndugu zangu wa Arusha, maendeleo hayana chama. Na ndio maana nilileta hapa bilioni 520 kwaajili ya maji, alisema Magufuli mbele ya umati wa wafuasi wa chama chake waliokusanyika mjini Arusha”

Lakini pia wakati huo huo amekuwa akisisitiza kuwa, ni vigumu kushirikiana na wabunge au madiwani kutoka vyama vingine katika kuleta maendeleo na hivyo, wananchi wakichagua wawakilishi ambao hawatokani na chama chake kama atapata ridhaa ya kuwa Rais, ni vigumu kushirikiana nao kuleta maendeleo katika maeneo yao jambo ambalo linapingana na kauli yake ya maendeleo hayana vyama.

Tansania Wahlplakate von John Magufuli
Wafuasi wa Magufuli wakimsikiliza kwenye mkutano wa kampeni.Picha: Daniel Hayduk/AFP/Getty Images

Som pia:Kampeni Tanzania zaingia ngwe ya lala salama 

"Mnichagulie wabunge na madiwani watakaoweka mawasiliano ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi. Na ndio maana ndugu zangu wana Arusha nimekuja hapa, niwaombe sana, tumechelewa sana ndugu zangu wa Arusha, tumechelewa ndugu zangu. Tumechelewa kwa sababu tunatakiwa tuwe na watu wenye uchungu na wananchi wa hapa”.

Pamoja na hayo Magufuli ambaye ana ushawishi mkubwa ndani ya chama cha CCM, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake baadhi ya mambo ambayo amefanikiwa kuyashughulikia katika mkoa wa Arusha ni pamoja na kujenga barabara za kiwango cha lami na kuboresha mioundombinu ya afya na kwamba kama atapewa ridhaa, serikali yake itajenga jengo la huduma za uchunguzi wa afya daraja la kwanza.

Tansania Wahlplakate von John Magufuli
Magufuli amewaomba wakaazi wa Arusha wampe fursa awafanyie mambo makubwa.Picha: Daniel Hayduk/AFP/Getty Images

Soma pia: Chadema: Utafiti unaomuweka Magufuli kifua mbele ni propaganda

"Lakini kwa maoni ninavyosikiliza kuna sera zilizonivutia, naitakia nchi yangu amani uchaguzi uwe wa huru na haki. Mpaka sasa nimeshajua nani anaweza kuiongoza Tanzania kura yangu ni ya muhimu sana, na kura yangu ni siri yangu," alisema mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano wa Magufuli.

Soma: CCM, na CUF zaendelea na kampeni za urais Tanzania

Japo kuna vyama zaidi ya 10 vilivyosimamisha wagombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Dr. John Pombe Magufuli, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani katika taifa hili la Afrika mashariki Tundu Lissu.

Mwandishi: Veronica Natalis