1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama nchini Kenya yatishia kumwachia huru Paul Mackenzie

10 Januari 2024

Mahakama nchini Kenya imetoa siku 14 kwa serikali kumfungulia rasmi mashtaka mchungaji Paul Mackenzie na watuhumiwa wengine 28, huku ikionya kuwa baada ya muda huo huenda ikalazimika kuwaachia huru.

https://p.dw.com/p/4b2n8
Kenia Kilifi | Miili ya waliokuwa waumini wa Paul Mackenzie iliyofukuliwa huko Shakahola
Polisi na vikosi vya uokoaji vikipakia kwenye gari miili ya waliokuwa waumini wa Paul Mackenzie iliyofukuliwa huko Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Kenya:22.04.2023Picha: Stringer/REUTERS

Hakimu Mkuu wa kitongoji cha Shanzu huko Mombasa, Yusuf Shikanda amebainisha kuwa washukiwa hao wamezuiliwa kwa siku 117 tangu maombi ya mwisho ya kuongeza muda wao wa kukaa rumande na kusema muda huo unatosha kukamilisha uchunguzi.

Upande wa utetezi umesema haki ya kikatiba ya kuachiliwa kwa dhamana mchungaji Mackenzie na watuhumiwa wengine imekiukwa kwa kuwa bado hawajashtakiwa.

Soma Pia: Mackenzie kusalia kizuizini miezi sita zaidi

Hakimu Shikanda amesema washukiwa hao wamezuiliwa bila kufikishwa mahakamani kwa muda mrefu kuliko mtu yeyote nchini Kenya tangu kupitishwa kwa katiba ya nchi hiyo mnamo mwaka 2010, inayopiga marufuku kumuweka mtu kizuizini bila kufunguliwa mashtaka.

Kenya-Kilifi | Miili ya waumini wa Paul Mackenzie ikifukuliwa huko Shakahola
Polisi na vikosi vya uokoaji vikipakia kwenye gari miili ya waliokuwa waumini wa Paul Mackenzie iliyofukuliwa huko Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Kenya:22.04.2023Picha: Stringer/REUTERS

Mackenzie ambaye amezuiliwa tangu Aprili 14 mwaka jana kutokana na vifo vya mamia ya watu ambao walikuwa wafuasi wa Kanisa lake la kiinjili la "Good News International "aliowarubuni kujinyima chakula ili waweze kwenda mbinguni kukutana na Yesu.

Hata hivyo Mackenzie anatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa tofauti la kupatikana na hatia ya kutumia studio na kutengeneza filamu bila ya kuwa na leseni halali.

Soma zaidi: Mahakama Kenya yaamuru Mackenzie kubakia rumande

Sakata hilo la kidini liliibuka wakati polisi walipowaokoa waumini 15 waliokuwa wamedhoofika kutoka katika kanisa la Mackenzie katika kaunti ya Kilifi kusini mashariki mwa Kenya.

Katika tukio la kutisha na lililogonga vichwa vya habari, miili ya karibu watu 429 ilifukuliwa katika msitu wa Shakahola karibu na pwani ya Bahari ya Hindi.

(Vyanzo: AP,AFP)