Mahakama Uganda yahalalisha ushindi wa Museveni
31 Machi 2016Shauri hilo liliwasilishwa na mgombea wa upinzani Amama Mbabazi, ambaye alitoa hoja za kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura, vitisho na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani. Shauri hilo pia linadai kuwepo na ushahidi wa udanganyifu, ikiwa ni pamoja na kupiga kura mara nyingi, na kuundwa kwa vituo haramu vya kupigia kura Februari 18.
Jaji Mkuu wa Uganda Bart Katureebe alikataa pingamizi hilo, akisema hakukuwa na ushahidi kwamba ushindi wa Museveni ulikuwa wa udanganyifu. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 alieitawala Uganda tangu 1986, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia karibu 61 ya kura.
"Tume ya uchaguzi ilimtangaza Museveni kihalali kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa rais," alisema Jaji mkuu Katureebe wakati akisoma hukumu mbele ya mahakama iliyokuwa imefurika mjini Kampala. "Hatuoni ushahidi wowote wa kuridhisha kuhusiana na madai ya kupiga kura mara nyingi," aliongeza, na kukataa madai ya upinzani ya kuwepo na vituo tofauti vya kujumlisha kura za uongo.
"Hakukuwepo na vituo haramu vya kujumlisha matokeo ambavyo tume ya uchaguzi ilipokea matokeo kutoka kwake," ilisema hukumu hiyo.
Ulinzi waimarishwa Kampala
Polisi waliojihami kwa silaha nzito walitawanya mjini Kampala kuzuwia maandamano ya vurugu ya wafuasi wa upinzani kupinga hukumu hiyo. Mwandishi wa DW mjini Kampala Lubega Emmanuel ameripoti kuwa jeshi hilo lilitumia nguvu kuwatawanya wafuasi kadhaa wa upinzani waliokuwa wameanza kujikusanya katika maeneo mbalimbali ya jiji kuandamana.
Mgombea alieshika nafasi ya tatu Amama Mbabazi, waziri mkuu wa zamani alieshinda juu ya asilimia moja tu ya kura, aliwasilisha pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi, lakini jopo la majaji tisa wa mahakama ya juu kabisaa nchini Uganda limelikataa pingamizi hilo kwa kauli moja.
"Tunapata tabu kuamini kuwa mafanikio finyu ya mlalamikaji kwenye vituo vya kupigia kura yalitokana na kutokuwepo kwa mawakala wake," ilisema hukumu hiyo.
Mpinzani wa karibu zaidi wa Museveni, Kizza Besigye, alikamatwa mara kadhaa wakati wa kampeni za uchaguzi na katika siku ya uchaguzi yenyewe, jambo ambalo alisema lilimzuwia kuwasilisha pingamizi sawa la kisheria. Anaendelea kuzuwiwa katika kifungo cha nyumbani. Polisi inasema yuko chini ya "kifungo cha uzuwiaji" ili asichochee vurugu.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Badru Kiggundu, ambaye pia ndie alisimamia chaguzi mbili zilizotangulia, ambazo Museveni alishinda, alitoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo.
Kiggundu aliomba radhi mahakamani kwa matatizo mengi yaliowakabili wapigakura katika mji mkuu and wilaya jirani ya Wakiso, zote zikiwa ngome kuu za upinzani, ambako vifaa vya kupigia kura vilipelekwa kwa kuchelewa au kutofikishwa kabisaa.
Ukosoaji
Chini ya sheria ya uchaguzi ya Uganda, mtu anaedai kuwepo na kasoro na kutaka matokeo ya uchaguzi wa rais yafutwe, anapaswa kuthibitisha kwamba kasoro hizo ziliathiri matokeo kwa kiasi kikubwa. Mashauri mawili sawa yaliowasilishwa na Besigye mwaka 2001 na 2006 akitaka kubadilitishwa kwa ushindi wa Museveni yalitupiliwa mbali kwa misingi sawa na kusababisha ukosoaji mkubwa.
Baadhi ya serikali za mataifa ya magharibi yaliomsifu Museveni huko nyuma kwa kusaidia mapambano dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia, zimemkosoa hivi karibuni kwa ukandamizaji dhidi ya wakosoaji wake na kuwanyanyasa wapinzani.
Mchambuzi wa siasa nchini Uganda Nicholas Ssengoba, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa ushindi wa Museveni unaakisi ugumu ulioukabili upinzani katika kukusanya ushahidi.
Mara baada ya shauri kuwasilishwa mahakamani, wezi walivunja ofisi mbili za mawakili wa Mbabazi na kuiba baadhi ya ushahidi. Mbabazi alisema wizi huo yumkini ulipangwa na jeshi la polisi, tuhuma ambazo serikali ilizikanusha.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre,afpe
Mhariri: Saumu Yusuf