Nigeria: Mahakama yaidhinisha ushindi wa rais Tinubu
26 Oktoba 2023Jopo la majaji saba wa Mahakama ya Juu limetupilia mbali rufaa iliyokatwa na upande wa upinzani iliyoupinga ushindi wa Tinubu kwa madai kwamba uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu, ukiukaji wa sheria za uchaguzi na kutozingatiwa vigezo vya kutokuwepo uhalali wa Tinubu kugombea uchaguzi.
Akitangaza uamuzi huo wa mahakamaJaji John Inyang Okoro amesema .''Baada ya kusuluhisha masuala yote dhidi ya rufani, maoni yake ni kuwa hakuna uhalali katika rufaa iliyokatwa na wameitupilia mbali.
Soma zaidi: Upinzani utakata rufaa kupinga urais wa Tinubu Nigeria
Mbali na ombi walilowasilisha awali, timu ya wanasheria wa Atiku pia ilikuwa imetaka kuwasilisha ushahidi mpya kwa Mahakama ya Juu, ambayo ilidai inaonyesha kuwa Tinubu aliwasilisha cheti cha kughushi kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Chicago, kama sifa ya kuhitimu elimu ya juu kwa tume ya uchaguzi alipotuma maombi yake ya kugombea urais.
Mwezi uliopita Mahakama ya Rufaa ya Uchaguzi iliwasilishiwa maombi mawili kutoka vyama vikuu vya upinzani, wakieleza madai ya udanganyifu, ukiukwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na madai kuwa Tinubu hakukidhi matakwa ya kikatiba kushiriki kinyang'anyiro hicho. Lakini nayo ilitupilia mbali.
Tinubu: Matumaini mapya kwa Nigeria
Tinubu, alieingia madarakani mwezi Mei na kauli mbiu ya "Matumaini Mapya" huku akiahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi haraka, amewataka Wanigeria kuweka kando tofauti zao.
Kwa mujibu wa Tinubu, ushindi huo umemtia nguvu zaidi na kuimarisha dhamira yake ya kuendelea kuwatumikia Wanigeria wote wa itikadi zote za kisiasa, makabila na imani. Tinubu pia amesema wao ni wa taifa moja hivyo ni wakati sasa kuendelea kufanya kazi na kujenga nchi kwa pamoja.
Wanaigeria wengi bado wanalalamikia kupanda mara tatu kwa bei ya mafuta na gharama za chakula kuwa kubwa, licha ya Utawala wa Tinubu kusitisha ruzuku ya mafuta na kujaribu kuimarisha sarafu ya naira mageuzi ambayo serikali yaNigeria imesema yatasaidia kukuza uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na kuvutia zaidi uwekezaji wa kigeni.
Kando na mageuzi ya kiuchumi, serikali yaTinubu pia inajaribu kukabiliana na changamoto kubwa za kiusalama, kutoka kwa waasi wa muda mrefu wa wanajihadi Kaskazini Mashariki, magenge ya utekaji nyara na mapigano ya kijamii katika maeneo mengine ya nchi humo.