Maji ya Fukushuma:China yamuita balozi wa Japan
16 Aprili 2021Mazungumzo hayo yalikuwa kati ya msaidizi wa waziri wa mambo ya kigeni wa China Wu Jianghao na balozi Hideo Tarumi ambapo kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya China, Japan inatuhumiwa kukiuka sheria ya kimataifa.
Serikali ya Japan inasisitiza kuwa kufunguliwa kwa maji kutoka katika mtambo huo ambao umekuwa ukihifadhi kiasi kikubwa cha maji kwa miaka mingi ni salama kwa sababu maji hayo yamesafishwa na kuondolewa mionzi yote. Lakini hatua hiyo ambayo haikutegemewa kuanza kwa miaka kadhaa sasa, tayari imechochea wasiwasi kutoka katika mataifa jirani na jamii za wavuvi.
China iliikosoa Japan Jumanne kwa uzembe mkubwa na kulalamika kuwa mpango huo utaathiri afya ya umma. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China, Wu Jianghao aliitaka Jaopan iache kumwaga maji hayo ya kemikali baharini kabla ya kuwa na makubaliano na wadau pamoja na mashirika ya kimataifa. Wu amesema uamuzi huo "siyo jambo linaloweza kufanywa na nchi ya kisasa iliyostaarabika".
Takribani tani milioni 1.25 za maji zimekuwa zikihifadhiwa kwenye matenki katika mtambo huo wa Fukushima ambao uliharibiwa baada ya ajali akubwa ya nyuklia, iliyosababishwa na tetemeko kubwa na tsunami Machi 11, 2011.
Ni hatua isiyozuilika
Waziri mkuu wa Japan Yoshihide Suga alisema kwamba kuyamwaga maji hayo ni zoezi lisilozuilika katika mchakato wa miongo kadhaa kuufunga mtambo huo wa nyuklia
Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki IAEA limekubaliana na kuachiwa huko kwa maji baharini ambapo linasema ni sawa na utiririshaji mwingine wowote wa maji taka unaofanywa na vinu vya nyuklia popote pale ulimwenguni.
Wakati huohuo, wachuuzi wa samaki wa Korea kusini katika mji mkuu Seoul pamoja na viongozi wa vyama vya upinzani wameitaka serikali ya ichukue hatua ya kuifanya Japan iachane na mpango wake wa kuyatiririsha maji yenye kemikali baharini kutoka katika mtambo huo wa nyuklia wa Fukushima ulioharibika. Jumatano, Rais wa Korea kusini Moon Jae-in aliwaamuru maafisa watafute amri ya mahakama ya kuizuia Japan kuyamwaga maji hayo baharini.