1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Gaza yaendelea, Israel yaishambulia Jenin

22 Januari 2025

Makubaliano legelege ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yanaendelea kutekelezwa, huku Israel ikiendelea na oparesheni yake ya kijeshi kwenye Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/4pSUX
Israel, Jenin, Palestina
Magari ya kijeshi ya Israel kwenye eneo la Jenin, Ukingo wa Magharibi.Picha: Mohammed Nasser\apaimages/IMAGO

Vikosi vya jeshi la Israel vikisaidiwa na helikopta vimeuvamia mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi tangu Jumanne (Januari 21)  na kuwauwa kwa uchache Wapalestina wanane katika kile Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alichokiita "operesheni kubwa, pana na muhimu ya kijeshi."

Operesheni hiyo ilianzishwa siku moja tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuondosha vikwazo walivyowekewa walowezi wa Kiyahudi wenye siasa kali za mrengo wa kulia, ambao wamekuwa wakiwashambulia na kuwauwa wanavijiji wa Kipalestina kwenye Ukingo wa Magharibi. 

Kwa mujibu wa Netanyahu, operesheni hii ni mashambulizi mapya dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.

Soma zaidi: Mkuu wa jeshi la Israel Meja Jenerali Herzi Halevi amejiuzulu

Maafisa wa usalama wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi.
Maafisa wa usalama wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi.Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP

Raia kadhaa wa Kipalestina kwenye Ukingo wa Magharibi wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi hayo ya jeshi la Israel. Mmoja wao, Adel Besher, amesema jeshi la Israel linamshambulia kila wanayempata.

"Nililala mtaani, kwenye uwanja wa hospitali, wakati nyumba yangu ipo umbali wa mita 200 tu kutoka hapa. Sikuweza kuifikia. Kuna majeruhi wengi. Wanne kwenye hospitali ya Al-Amal walijeruhiwa, wakiwemo madaktari, wauguzi na wagonjwa. Watu wengine watatu ama wanne walijeruhiwa karibu na nyumba yangu na hakuna aliyeweza kuwaokowa. Wanajeshi wa Israel wanampiga risasi kila anayewakaribia, watu wawili walijeruhiwa wakati wakijaribu kuwaokowa." Alisema.

Jeshi la Israel lilisema vikosi vya jeshi, polisi na ujasusi vimeanza operesheni ya kupambana na kile lilichokiita ugaidi ndani ya Jenin, kufuatia wiki kadhaa za operesheni za vikosi vya usalama vya Mamlaka ya Palestina kurejesha udhibiti kwenye kambi moja ya wakimbizi, ambayo inadaiwa kuwa kituo kikuu cha makundi yenye silaha, wakiwemo Hamas na Islamic Jihad. 

Fidia ya kushindwa Gaza?

Hata hivyo, baadhi ya wakaazi wa Ukingo wa Magharibi wanasema kwa Israel kuzidisha kampeni yake ya kijeshi hivi sasa kwenye Ukingo wa Magharibi si jambo jipya wala la ajabu, baada ya kile wanachodai kuwa jeshi hilo lilishindwa kutimiza malengo yake hata baada ya kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa takribani mwaka mmoja na nusu.

Ukingo wa Magharibi, Jenin, Palestina
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin, Ukingo wa Magharibi.Picha: Raneen Sawafta/REUTERS

"Kile walichoshindwa kukifanikisha kwenye Ukanda wa Gaza, wanajaribu kukifidia hapa Jenin. Jenin ni jina la upinzani na mapambano. Wakiumaliza upinzani hapa Jenin, wataumaliza kwenye Ukingo wote wa Magharibi." Alisema Adil Besher.

Soma zaidi: Israel yatangaza kufanya operesheni maalum Gaza

Operesheni hii ya Jenin, ambako jeshi la Israel limefanya uvamizi mara kadhaa kwenye eneo hilo katika miaka ya karibuni, ilianza ikiwa ni siku mbili tu tangu kuanza utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na inaongeza kitisho cha machafuko zaidi kwenye Ukingo wa Magharibi. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal Bin Farhan amesema anatumai kuwa makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza yataheshimiwa na kwamba ni jukumu la wadau wote huko Mashariki ya Kati kuyadumisha makubaliano hayo.