Makubaliano ya kuvimaliza vita vya Gaza bado yasubiriwa
15 Januari 2025Qatar, Misri na Marekani zinaongeza juhudi za usuluhishi utakaowezesha kuvimaliza vita na kuachiliwa mateka waliochukuliwa wakati Hamas ilipofanya mashambulio mnamo Oktoba 7, mwaka 2023 kwenye ardhi ya Israel.
Kulingana na ofisi ya Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, walipoongea kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden waliweka mkazo juu ya Israel na Hamas kuonyesha maridhiano ili kufanikisha kupatikana makubaliano ya kuvimaliza vita katika Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema kiongozi huyo alikutana na wakuu wa usalama jana usiku. Hata hivyo, iwapo makubaliano yatafikiwa, hayataanza mara moja.
Kwa sababu mpango huo utahitaji kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri la Usalama la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kisha uwasilishwe kwenye Baraza lake kamili la Mawaziri kwa ajili ya kuidhinishwa. Idadi kubwa ya mawaziri katika mabaraza yote mawili ni washirika wa Netanyahu na hivyo uwezekano wa kuidhinisha pendekezo lolote analowasilisha ni mkubwa.
Soma Pia: Qatar yasema mazungumzo ya usitishwaji vita Gaza yako hatua za mwisho
Ingawa mara kadhaa kumekuwepo na matumaini kama hayo, mazungumzo yamekuwa yakisambaratika mara kwa mara huku pande mbili za Israel na Hamas ziktupiana lawama, lakini kuna matumaini makubwa safari hii makubaliano yatapatikana kabla ya tarehe 20 Januari ambapo Rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuapishwa kuwa rais na pia anawakilishwa na mjumbe wake katika mzungumzo ya mjini Doha.
Wakati huo huo, ndugu na jamaa za watu waliotekwa nyara mnamo Oktoba 7 walikutana hii leo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Gil Dickmann ni mmoja wao amesema wanataka makubaliano yafikiwe yatakayowezesha mateka wote kuachiliwa na sio kwa awamu ingawa hadi sasa ni mateka walio katika orodha ya awamu ya kwanza tu ndio watakaoachiliwa.
Katika awamu hiyo ya kwanza ya kusimamisha vita, Hamas itawaachia huru mateka 33 wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza, na Israel itawaachilia wafungwa wapatao 1,000 wa Kipalestina.
Soma Pia: Makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza yanukia
Kwingineko Norway ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa utekelezaji wa suluhisho la kupatikana mataifa mawili ya Israel na Palestina. Mkutano huo unafanyika mjini Oslo, na unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Espen Barth Eide.
Akihutubia kwenye mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Mohammad Mustafa, amesema sasa ni nafasi muhimu ya kuchukua hatua madhubuti katika mkutano wa Norway.
Mpango huo ulizinduliwa na Norway, Umoja wa Ulaya na Saudi Arabia wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York Septemba mwaka uliopita. Madhumuni ya mkutano huo ni kubainisha hatua gani madhubuti ambazo nchi nyingi na mashirika yanayounga mkono suluhu ya kuwepo na mataifa mawili zinaweza kuchukua ili kuhakikisha kuwa zinatimizwa.
Norway ni mojawapo ya nchi tatu za Ulaya zilizolitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Mei.
Vyanzo: AFP/RTRE