1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya jeshi ya Kati yashambuliwa na makundi ya kigaidi

22 Julai 2022

Mali imethibitisha leo kuwa wanamgambo wa itikadi kali wameishambulia kambi ya kijeshi katika wilaya ya Kati, nje kidogo ya mji mkuu Bamako.Ni kwa mara ya kwanza kambi hiyo kushambuliwa na waasi hao.

https://p.dw.com/p/4EWlq
Mali Schüsse auf Militärstützpunkt in Kati
Picha: Fadimata Kontao/REUTERS

Kulingana na taarifa iliyotolewa na jeshi la Mali, magari mawili yaliyokuwa yamepakia mabomu yalilipua kambi hiyo alfajiri ya leo na kuwa jeshi lilizima shambulio hilo la kigaidi kwa nguvu zote kwenye kambi ya Kati na kusisitiza kuwa washambuliaji wawili waliuawa. Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa hali kwa sasa imedhibitiwa na msako unaendelea ili kuwatafuta wahusika na washirika wao.

Shambulio la leo kwenye kambi ya Kati linafuatia mfululizo wa mashambulizi ya waasi hao jana Alhamisi, ambapo katika moja ya matukio hayo, watu wenye msimamo mkali walikishambulia kituo cha polisi huko Kolokani, takriban kilomita 60 kaskazini mwa mji mkuu Bamako na wanajeshi wawili wa Mali waliuawa.

Soma zaidi: MINUSMA:Zaidi ya watu 500 wameuwawa Mali

Kiongozi wa utawala wa kijeshi unaoongoza nchini Mali Luteni Kanali Assimi Goita, mara kwa mara huweka makazi yake katika kambi hiyo ya Kati, ambako aliratibu mapinduzi ya mwaka 2020 na ambayo yalipelekea kuingia kwake madarakani.

Miaka 10 ya uasi wa kigaidi nchini Mali

Mali Kati | Armee Soldaten
Wanajeshi wa Mali wakikagua gari, katika mji wa Kati.Picha: Mohamed Salaha/AP Photo/picture-alliance

Wanamgambo wa itikadi kali wenye mafungamano na kundi la Al-Qaida na lile linalojiita Dola la Kiislamu IS, wamekuwa wakijizatiti katika uasi wao uliodumu kwa karibu miaka kumi. Mashambulizi yao mengi yamekuwa yakilenga eneo la kaskazini mwa Mali lakini hivi karibuni walijikita zaidi katikati mwa Mali na mwezi huu wamekuwa wakiukaribia mji mkuu Bamako.

Soma zaidi: ECOWAS yaziondolea vikwazo Mali na Burkina Faso

Mamlaka zimefahamisha kuwa wiki iliyopita watu wenye silaha walishambulia kituo cha ukaguzi cha jeshi kilicho umbali wa kilomita 60 nje ya Bamako, na kuua watu wasiopungua sita na kuwajeruhi wengine kadhaa. Hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, lakini inadhaniwa yaliendeshwa na kundi lenye mafungamano na al-Qaida linalojulikana kama JNIM.

Usaidizi wa kimataifa

Tangu mwaka 2012, Mali imekuwa ikijitahidi kuzuia uasi wa makundi yenye itikadi kali za Kiislamu. Waasi hao walichukua udhibiti wa miji ya kaskazini mwa Mali lakini walifurushwa kutokana na operesheni ya usaidizi wa kijeshi iliyoongozwa na Ufaransa.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa kimesema zaidi ya askari wake 250 wa kulinda amani pamoja na wafanyakazi wamepoteza maisha tangu mwaka 2013, na kuifanya Mali kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo katika jumla ya vikosi vyote vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa duniani kote.

Soma zaidi:Jumuiya ya ECOWAS kuendeleza vikwazo dhidi ya viongozi wa kijeshi wa Mali. 

Wiki iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ulitangaza kuwa ifikapo katikati mwa mwezi Agosti, Misri itajiondoa katika kikosi hicho cha kulinda amani ikitaja kuwa sababu kuu ni mashambulizi mabaya yanayosababisha vifo vya askari wake. Mvutano umekuwa ukiongezeka kati ya serikali ya kijeshi ya Mali na kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa.

(APE)