1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya watu wauawa Sudan Kusini

18 Desemba 2013

Umoja wa Mataifa umesema kati ya watu 400 na 500 wameuawa katika mapigano yaliyozuka Sudan Kusini, huku serikali ya nchi hiyo ikitangaza kuwakamata wanasiasa kumi wanaohusishwa na jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

https://p.dw.com/p/1Abmd
Wananchi wa Sudan Kusini wakiwa kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa
Wananchi wa Sudan Kusini wakiwa kwenye ofisi za Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/AA

Umoja wa Mataifa umepokea taarifa hizo kutoka katika duru za ndani ya mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kuongeza kuwa watu wengine 800 wamejeruhiwa, huku wengine kiasi ya 20,000 wakipewa hifadhi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Juba.

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi Gerard Araud amewaambia waandishi wa habari kuwa baraza hilo limepokea taarifa zinazotofautiana, wakati wa kikao chake jana jioni kutoka kwa mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous.

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Gerard Araud
Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Gerard AraudPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa bado haijathibitisha idadi hiyo

Hata hivyo baraza hilo la Umoja wa Mataifa halijazithibitisha taarifa kuhusu idadi kamili ya watu waliouawa.

Araud ambaye ni balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa amesema wana wasiwasi mkubwa huenda kukawa na idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa. Hospitali mbili zimeripoti kuwa kati ya watu 400 na 500 wameuawa na wengine zaidi ya 800 wamejeruhiwa.

Rais wa Salva Kiir wa Sudan Kusini
Rais wa Salva Kiir wa Sudan KusiniPicha: Reuters

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amesema mapigano hayo yanayotokana na jaribio la mapinduzi lililoshindwa, yamefanywa na wanajeshi watiifu kwa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.

Serikali ya Sudan Kusini imesema imewakamata wanasiasa kumi kwa tuhuma za kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi, huku ikiendelea kumtafuta Machar. Baadhi ya wanasiasa waliokamatwa ni pamoja na waziri wa zamani wa fedha, Kosti Manibe.

Machar akanusha kuhusika

Hata hivyo, Machar amekanusha kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi. Kauli hiyo imechapishwa leo katika gazeti moja la Sudan Kusini lenye makao yake mjini Paris, Ufaransa. Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na Machar tangu yalipozuka mapigano siku ya Jumapili.

Aufnahme des Südsudan in die Vereinten Nationen
Riek Machar akiwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-MoonPicha: dapd

Akizungumza kutoka eneo lisilojulikana, Machar amefafanua kuwa kilichotokea Juba ni suala la kutoelewana kati ya walinzi wa rais ndani ya ngome zao na siyo jaribio la mapinduzi. Ama kwa upande mwingine msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Kanali Philip Aguer amesema mapigano kati ya vikundi vya kijeshi yameenea hadi kwenye mji wa Jonglei.

Wakati huo huo Marekani imesema itawaondoa raia wake walioko Sudan Kusini kutokana na kuongezeka kwa mapigano na kwamba itasimamisha shughuli katika ubalozi wake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry ametoa wito wa kupatikana suluhisho kwa njia ya amani na kidemokrasia. Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano hayo na kuzitolea wito pande zinazopigana kusitisha mara moja uadui.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,DPAE,AFPE
Mhariri: Ssessanga Iddi