1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Manchester United yaahidi kufanya makubwa zaidi msimu ujao

27 Mei 2024

Wachezaji wa Manchester United wameahidi kufanya "mambo makubwa zaidi" msimu ujao katikati ya kiwingu kuhusu mustakabali wa kocha wao Erik ten Hag.

https://p.dw.com/p/4gLVj
Mlinda lango wa Manchester United Andre Onana akisherehekea na wachezaji wenzake baada ya kuokoa mkwaju wa penalti
Mlinda lango wa Manchester United Andre Onana akisherehekea na wachezaji wenzake baada ya kuokoa mkwaju wa penaltiPicha: PAUL ELLIS/AFP

Wachezaji wa Manchester United wameahidi kufanya mambo makubwa zaidi msimu ujao katikati ya kiwingu kuhusu mustakabali wa kocha wao Erik ten Hag.

Mashetani hao wekundu walichukua ubingwa wa Kombe la FA kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane baada ya makinda Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo kufunga mabao na kuipa ushindi klabu hiyo ya Old Trafford dhidi ya mahasimu wao wa jadi Manchester City.

Kombe la FA ni la pili kunyayuliwa na Erik ten Hag tangu alipochukua mikoba ya kuitia makali klabu hiyo.

Soma pia: Ten Hag asema mlango bado uko wazi kwa Sancho United 

Kocha huyo raia wa Uholanzi aliingia kwenye fainali dhidi ya Manchester City huku kukiwa na ripoti kwamba huenda akapigwa kalamu bila ya kujali matokeo ya mchezo huo.

Alipoulizwa kuhusu iwapo atasalia kuwa kocha wa Manchester United msimu ujao, Erik ten Hag amesema, "Sifikirii kuhusu hilo. Niko kwenye mradi na tuko mahali tunapopaswa kuwepo yaani, kuijenga upya timu. Nilipoingia hapa, timu ilikuwa mbaya mno na sasa tunaelekea kujenga timu imara ya siku zijazo. Na hilo kutokea, lazima kutakuwepo panda shuka."

Kocha wa Manchester United Erik ten Hag
Kocha wa Manchester United Erik ten HagPicha: Andrew Yates/Sportimage/Cal Sport Media/picture alliance/Newscom

Kwa upande wake, kocha Pep Guardiola amejilaumu kwa masaibu yalioikumba Manchester City katika fainali hiyo. Raia huyo wa Uhispania ameeleza kuwa mbinu zake uwanjani hazikufanya kazi.

Guardiola ameahidi kuwa timu yake itazidisha makali zaidi msimu ujao licha ya kipigo mbele ya jirani zao.

"Kwanza kabisa, naipongeza Manchester United kwa kushinda Kombe la FA. Nadhani mbinu yangu hasa kipindi cha kwanza, haikuwa nzuri. Tulikosa utulivu. Kipindi cha pili kilikuwa bora, tulicheza kwa ushirikiano, kwa sehemu fulani kwa sababu ya kufungwa 2-0. Unapokuwa chini, unacheza kwa tahadhari na kujaribu kurudi mchezoni. Ulikuwa mchezo mgumu. Hatukujilinda vizuri walipofunga bao la kwanza, na bao la pili lilifungwa kwa ustadi. Tulipaswa kuwa makini."

Kuna hali ya ati ati kuhusu mustakabali wa Pep Guardiola huku ripoti zikidai kuwa, huenda akaitosa Manchester City mwishoni mwa msimu ujao.

Guardiola, aliyejiunga na Manchester City miaka minane iliyopita amesalia na miezi 12 tu kwenye kandarasi yake na inaaminika kuwa mwaka ujao ndio huenda ukawa wake wa mwisho ndani ya Etihad.

Tayari majina kadhaa yameanza kuhusishwa na kibarua hicho akiwemo Roberto De Zerbi, Miguel Sanchez wa klabu ya Girona na hata Julian Nagelsmann anayeifunza timu ya taifa ya Ujerumani.