Maoni: Matokeo ya uchaguzi wa Italia na mzozo mpya EU
27 Septemba 2022"Tunashangiria pamoja na Italia," inasomeka twiti kutoka Ujerumani. Mbunge mmoja wa Ufaransa katika bunge la Ulaya aliandika kwamba Wataliano wameupa Umoja wa Ulaya somo la unyenyekevu.
Wanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia kote Ulaya wanamshangiria Giorgia Meloni.
Kiongozi huyo wa chama cha tawi la siasa kali za kizalendo, Fratelli d'Italia, ama Ndugu wa Italia, anaongoza pamoja na muungano wake wa siasa kali za mrengo wa kulia kwenye uchaguzi wa bunge na ana uwezekano mkubwa wa kuongoza serikali ijayo nchini humo.
Kwa Italia, ambayo ni miongoni mwa waasisi wa Umoja wa Ulaya, haya ni mageuko kabisa na sio mageuzi makubwa tu.
Hakuna wakati wowote tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, ambapo bunge la Italia limegeuka kuwa la siasa kali zaidi za mrengo wa kulia kuliko hili lililochaguliwa sasa.
Chama cha Ndugu wa Italia cha Meloni, ambacho chimbuko lake ni kwenye ufashisti mamboleo, kwa sasa ndicho chenye nguvu kubwa kabisa bungeni humo.
Kwa ushirikiano na chama chengine cha siasa kali za kizalengo, Liga, chake Matteo Salvini, na cha Forza Italia chake waziri mkuu wa zamani, Silvio Berlusconi, sasa wana wingi wa kutosha kuunda serikali.
Hasira za wapigakura
Mageuko haya kuelekea siasa kali za mrengo wa kulia nchini Italia, hapana shaka, kunahusiana sana na hali ya kisiasa nchini humo. Wataliano wengi hawafurahishwi na wanakerwa na tabaka la wanasiasa.
Robo moja ya wenye haki ya kupiga kura walijitenga kando na uchaguzi huo. Serikali tatu zimeshakuwa madarakani ndani ya kipindi cha miaka minne tu. Chama cha Giorgia Meloni hakikuhusika na hata moja kati ya hizo. Na sasa amefaidika na hali hiyo.
Mzozo wa nishati, upandaji wa bei za bidhaa muhimu, kile kinachoonekana kama kupoteza udhibiti wa wahamiaji, khofu kwa kesho yao - yote haya yamekuwa mambo ambayo mwanasiasa huyo mwenye mvuto kwa siasa kali za mrengo wa kulia aliyaona kama fursa na kuyatumilia kwenye kampeni zake.
Akawaahidi watu kwamba atakayashughulikia. Kwa kuwa hicho hasa ndicho Wataliano wengi walichotaka kukisikia. Tabaka la wanasiasa mjini Rome lilikuwa limeyasahau kabisa hayo, tabaka ambalo raia wengi wanaliona kama klabu ya kujitajirisha wenyewe tu.
Lakini Umoja wa Ulaya pia unalaumiwa kwa hali hii mbaya. Kwa wengi nchini Italia ni chombo kisicho maana, chenye utata, kilichojikita kwenye kuzingatia maslahi ya walio serikalini tu na kilichojitenga mbali sana watu wa kawaida kwenye nchi wanachama.
Hapa ndipo hasa Giorgia Meloni alipoanzia lugha yake ya kisiasa. Na ndipo alipofanikiwa.