1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais Xi wa China, Putin wa Urusi waibua changamoto kwa G7

Daniel Gakuba
12 Desemba 2021

Mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la G7 la nchi za kidemokrasia zilizositawi kiviwanda unamalizika Jumapili mjini Liverpool, Uingereza. Ingawa Urusi na China sio wanachama wa kundi hilo zimekuwa agenda muhimu ya mjadala.

https://p.dw.com/p/449u9
Liverpool G7 Außenminister Treffen
Picha ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kundi la G7Picha: Olivier Douliery/Pool/REUTERS

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameibua mjadala mkubwa miongoni mwa nchi za magharibi baada ya hatua yake ya kuyasogeza maelfu ya wanajeshi wa Urusi na vifaa vya kivita karibu na mpaka wa Ukraine. Washirika wa kundi la G7 ambao wengi wao pia ni wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wana wasiwasi kuwa huenda Urusi inaweza kuivamia Ukraine kijeshi, na wameionya serikali ya Rais Putin kuwa itakabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi iwapo itaishambulia Ukraine.

Soma zaidi: Mawaziri wa Nje wa G7 wakutana kuionya Urusi

Pamoja na kwamba Urusi ndio ilikuwa na nafasi ya kwanza kujadiliwa kutokana na kujitutumua kijeshi, China pia inazipa homa kali nchi za G7, kutokana na kasi yake ya ukuaji wa kiuchumi na kujiimarisha kijeshi katika muda wa miaka 40 iliyopita.

Kuhusu Urusi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani na wenzake wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan wameunga mkono kauli ya Rais Joe Biden kwa Rais Vladimir Putin, alipomuonya kutothubutu kuivamia Ukraine katika mazungumzo yao kwa njia ya video.

Russland Taganrog | Militär-Manöver nahe Grenze Ukraine
Urusi imekuwa ikijiimarisha kijeshi karibu na mpaka wa Ukraine, ikiaminika kurundi wanajeshi zaidi ya 100,000Picha: REUTERS

Muafaka kuhusu msimamo mkali, tofauti kuhusu hatua za kuchukua

Afisa mmoja mwandamizi wa wizara ya nje ya Marekani amesema ''sio jambo la kufurahisha, lakini iwapo Urusi itaishambulia Ukraine, hatutakuwa na budi bali kujibu kwa vikwazo vikali kabisa vya kifedha na vya kiuchumi dhidi ya Urusi.''

Urusi imekanusha kuwa na mipango ya kuishambulia Ukraine, lakini inataka ipatiwe uhakika wenye uzito kisheria, kwamba jumuiya ya NATO haitaendelea kujitanua upande wa mashariki mwa Ulaya.

Soma zaidi: Biden na Putin wafanya mazungumzo kwa njia ya mtandao

Hata hivyo, licha ya kuungana kwa kauli ya kuilaani mipango ya Urusi dhidi ya Ukraine, hakuna makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo wa G7 kuhusu hatua thabiti za kuchukua iwapo Ukraine itavamiwa, mojawapo ya tofauti kati ya washirika hao ikihusu bomba la gesi la chini ya bahari linaloziunganisha Urusi na Ujerumani, la Nord Stream 2, hii ikiwa ni kwa mujibu wa duru zenye taarifa za ndani za mkutano huo wa Liverpool.

Lakini hata kama Rais Putin ndiye mwiba mchungu kwenye unyayo wa G7 kwa wakati huu, kitendawili kigumu zaidi kwa kundi hilo ni mwenzake wa China China Xi Jinping. Afisa mmoja aliyehudhuria mkutano wa Liverpool amesema ''muda mwingi ulitumika kuizungumzia kwa kina China''.

China | Shenzhou-13 Raumfahrtmission
Kukua haraka kwa China kiuchumi na kijeshi kunazikosesha usingizi nchi za kundi la G7Picha: AFP/Getty Images

Kuimarika kwa China ni 'umiza kichwa' kwa G7

Kuibuka kwa China kama taifa kubwa kiuchumi duniani kunatazamwa na wachambuzi kama tukio kubwa zaidi katika siasa za uchumi na uzani wa nguvu duniani, tangu kusambaratika kwa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991 na kumalizika kwa vita baridi.

Mwaka 1979, uchumi wa China ulikuwa mdogo kuliko wa Italia, lakini baada ya kuufungua uchumi wake kwa wawekezaji wa nje na kuanzisha mageuzi kwenye soko lake, imepiga hatua kwa kasi na kuwa ya pili yenye uchumi mkubwa duniani baada ya Marekani, na miongoni mwa nchi zinazoongoza katika sekta ya teknolojia.

China ambayo haijawahi kuwa mwanachama wa kundi la G7 lililoasisiwa mwaka 1975, mwezi Juni ililikejeli kundi hilo, ikisema enzi za dunia kufuata maelekezo ya kundi la ''viji-nchi vidogo'' imepita na itabaki kuwa historia.

''Ni suala muhimu kwamba hivi sasa ukanda wa Indo-Pasifiki ndio wenye kuangaziwa zaidi'', amesema afisa mwingine wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Soma zaidi: Ukraine yaitaka NATO kuyakataa madai ya Urusi

Chanzo kingine kutoka mkutano wa mawaziri wa nje wa nchi za G7 amesema hali ya Hong Kong, mkoa wa Xijiang na mvutano na Taiwan ilimulikwa sana na mawaziri.

Mawaziri hao pia wamejadili msaada wa Lithuania, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambayo imeikasirisha China kwa kuiruhusu Taiwan kufungua ofisi ya kibalozi, na China ikajibu kwa kushusha hadhi ya mahusiano yake na taifa hilo la ukanda wa Baltiki.

Mwenyeji wa mkutano huo wa G7, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss, amesema wametuma ujumbe kwamba watasimama kidete dhidi ya mienendo ya ubabe wa China, akisisitiza hata hivyo kuwa mkutano wao haukuwa na azma ya uhasama kwa China.

 

rtre,ape