Marekani, Japan zakubaliana kuimarisha ushirikiano
7 Januari 2022Mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Marekani na Japan walifanya mazungumzo kwa njia ya mtandao leo Ijumaa, wakielezea wasiwasi wao kuhusu China.
Washington iliwakilishwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken. Kwa upande wa Japan walikuwa Waziri wa Ulinzi Nobuo Kishi na Waziri wa Mambo ya Nje Yoshimasa Hayashi.
Wawakilishi hao wa nchi hizo mbili wamesisitiza umuhimu wa muungano wa usalama wa Marekani na Japan huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uthubutu wa kikanda wa Beijing na ukandamizaji ndani ya mipaka yake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema nchi hizo mbili zilifikia makubaliano mapana juu ya mkataba mpya wa miaka mitano kuhusu kugawana gharama za uwepo wa jeshi la Marekani nchini Japan.
Pia amesema Washington na Tokyo zitatia saini mkataba juu ya utafiti na maendeleo ya teknolojia zinazohusiana na ulinzi, ikiwa ni pamoja na njia za kukabiliana na vitisho vya silaha za kisasa na hatari zaidi.
Muungano huo kama nguzo ya amani
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imesema mkutano huo umesisitiza umuhimu wa Muungano wa Marekani na Japan kama "nguzo ya amani na ustawi katika kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki"
Austin na Blinken wamesema wamejitolea kuendelea na ushirikiano wa karibu na washirika wao wa Japan ili kuboresha na kuimarisha muungano wao.
Katika kuashiria matarajio ya China katika eneo hilo, Waziri wa mambo ya kigeni wa Japan amesema "kuna umuhimu zaidi" kwa Japan na Marekani "kuungana na kuonyesha uongozi bora" ili kukabiliana na changamoto kadhaa.
Blinken alinukuliwa na shirika la habari la Japan, Kyodo, akisema ni muhimu kuwa makini na nchi zinazotaka kuhujumu utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria. Maoni hayo yalidhaniwa kuzilenga China na Korea Kaskazini.
Ushirikiano ili kudumisha haki za binaadamu
Wajumbe katika mkutano huo wametoa taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo na kusema "wameamua kufanya kazi pamoja ili kuzuia na ikihitajika, kukabiliana na shughuli zinazovuruga eneo hilo," Viongozi hao wamedhihirisha "wasiwasi mkubwa" kuhusu masuala ya haki za binadamu katika mkoa wa Xinjiang wa China, na pia huko Hong Kong. Taarifa hiyo pia imesisitiza umuhimu wa amani na utulivu huko Taiwan.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa China Wang Wenbin amesema kwamba China inasikitishwa na maoni ya Marekani na Japan na kusema imewasilisha malalamiko rasmi kwa nchi zote mbili, amesema Wang, katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari huko Beijing.