1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kupeleka ndege za kivita Libya

Halima Nyanza(ZPR)22 Aprili 2011

Marekani imetangaza kutumia ndege zinazojiendesha zenyewe dhidi ya Libya kusaidia juhudu zinazofanywa na jeshi la muungano wa kimataifa nchini humo.

https://p.dw.com/p/112H5
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert GatesPicha: UNI

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na hali ya kibinadamu.

Ndege hizo zinazojiendesha zenyewe bila ya rubani, zinategemewa kutumiwa kutokana na uwezo wake wa kupaa umbali mdogo na kuweza kuwa na upeo mzuri wa kuona wanacholenga.

Wakati huohuo waasi nchini Libya wamechukua udhibiti wa eneo muhimu la mpaka wa nchi hiyo na Tunisia baada ya mapambano makali na jeshi linalomuunga mkono kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Libyen Misrata Brand Fabrik Aufstand
Mapigano yalivyouharibu mji wa MisrataPicha: picture alliance / dpa

Shirika la habari la Tunisia limeripoti kuwa maafisa kadhaa na wanajeshi ambao wamekimbia, mapigano hayo walijisalimisha wenyewe kwa jeshi la Tunisia mpakani.

Ushindi huo wa waasi umekuja wakati ambao, majeshi ya Gaddafi yakiendelea na mashambulio makali katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Misrata, ambako maelfu ya raia walihamishwa jana katika mji mkuu wa waasi wa Benghazi ulioko mashariki.