1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuweka sheria mpya kuzuia dhulma za polisi?

8 Juni 2020

Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani hii leo wanapanga kuzindua muswada mpana wa kisheria unaolenga kuzuwia vurugu za polisi na dhulma za ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/3dSF5
Washington: Das Kapitol - Sitz des US-Kongresses
Picha: picture-alliance/J. Schwenkenbecher

Hii ni baada ya wiki mbili za maandamano kote nchini humo, yaliyochochewa na kifo cha George Floyd akiwa mikononi mwa polisi wa Minneapolis. 

Kulingana na chanzo cha bunge, pendekezo hilo linatarajiwa kuweka zuio kwa polisi kumkandamiza mtu shingoni na kumfanya ashindwe kupumua, kutumia rangi ama kabila kama msingi wa kumtuhumu mtu kufanya uhalifu, polisi nchini humo kuvaa camera pamoja na kuondoa kanuni ya kisheria ambayo humpa kinga afisa wa serikali kuchukuliwa hatua za kisheria na raia.

Mwakilishi wa mwenyekiti wa umoja wa wabunge weusi Karen Bass amekiambia kituo cha utangazaji cha CNN hapo jana kwamba muda umefika  kwa idara za polisi kubadilika. Ameongeza kuwa ana matarajio wimbi la maandamano makubwa ya amani lililoonekana kote Marekani wiki mbili ziliziopita huenda likaongeza shinikizo kwa wabunge kuchukua hatua.

USA Protest nach dem Tod von George Floyd | Präsident Trump auf dem Weg zur St John's Episcopal  Kirche
Haijulikani kama rais Trump atakubaliana na muswada huo wa mageuziPicha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Bado haiko wazi hata hivyo iwapo pendekezo hilo litaungwa mkono na wabunge wa Republican wanaolidhibiti baraza la seneti. Uungaji wao mkono pamoja na ule wa rais Donald Trump ambaye pia ni Mrepublican utahitajika sana ili muswada huo uweze kuwa sheria.

Nchini Afrika Kusini, wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters, EFF wameandamana kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi, wakiungana na kampeni ya kimataifa ya Black Lives Matter. Takriban watu 200 wameandamana mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Pretoria wakipiga kelele za kupinga ubaguzi, rais Donald Trump na ubeberu.

Kiongozi wa EFF, Julius Malema amewaambia waandamanaji hao waliopiga magoti kwa dakika 8.46 kuashiria muda aliokandamizwa Floyd, akisema imetosha kwa vitendo vya ukatili wa polisi kwenye miili ya watu weusi na kuahidi kushikama na Wamarekani weusi katika kipindi hiki kigumu.

red beret - Der EFF-Vorsitzende Malema stellt die Parteipläne vor SONA JOHANNESBURG SOUTH AFRICA vor
Kiongozi wa EFF, Julius Malema, amekosoa dhulma hizo na rais Donald TrumpPicha: imago/Gallo Images

Alisema, "Wamarekani walikuwa nasi tulipokuwa tunakabiliwa na wakati mgumu, harakati za kupinga ubaguzi huko Marekani ziliongozwa na Wamarekani weusi wenyewe, na wanapopitia kipindi kigumu ni muhimu sisi pia tushikamane nao."

Malema pia amemkosoa rais Trump akimtaja kama mwakilishi wa kile alichotaja kama ubeberu wa kizungu.

Nchini Ufaransa nako waandamanaji wameendelea kupinga ubaguzi lakini sasa wakimtaja kijana Adama Traore aliyefariki kwa ukatili sawa na aliofanyiwa Floyd. Dada yake Assa Traore, amesema Adama alikandamizwa na polisi watatu. Adama alikuwa anasherehekea siku ya kuzaliwa Julai 19, 2016 wakati polisi walipomfanyia ukatili huo, na wakati anafikishwa kituo cha polisi, alikuwa hajitambui na haikuwezekana kurudi katika hali ya kawaida.

Kifo chake kilichochea maandamano makubwa nchini Ufaransa, ambako ukatili wa polisi na ubaguzi havizungumziwi.

Mashirika: RTRE/AFPE