Miito yaongezeka ya kumwondoa Trump madarakani mapema
8 Januari 2021Rais wa Marekani Donald Trump amesema amekasirishwa na watu hao ambao ni wafuasi wake waliotumia nguvu na kufanya vurugu ndani ya ofisi za bunge baada ya kulivamia. Trump amesema watu hao waliyahujumu makao makuu ya demokrasia ya nchini Marekani na ameeleza kuwa waliofanya vurugu hizo wanapaswa kulaaniwa na kuadhibiwa.
Rais Donald Trump kwa mara ya kwanza amekiri kwamba Joe Biden ni rais ajae wa Marekani, ametamka hayo siku moja baada ya wafuasi wake kuvamia bunge wakati lilipokuwa linajiandaa kuthibitisha ushindi wa Biden. Trump amesema la muhimu sasa ni kuhakikisha kuwa zoezi la kubadilishana madaraka linakwenda vizuri.
Soma Zaidi:Wabunge wa Marekani wauidhinisha ushindi wa Joe Biden
Kauli hiyo imeonesha ugeugeu wa Trump tofauti na Trump yule aliyetumia miezi kadhaa akisisitiza kuwa alishindwa kwenye uchaguzi wa Novemba 3 kutokana na udanganyifu uliotokea, bila ya kutoa ushahidi. Trump ametoa matamshi hayo baada ya wabunge wa vyama vyote viwili pamoja na viongozi waandamizi katika utawala wa rais huyo kuanza mazungumzo juu ya kumwondoa madarakani.
Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema ikiwa hataondolewa kwa njia ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya Marekani basi bunge litajaribu kwa mara ya pili kumfungulia mashtaka juu ya kumwondoa madarakani. Spika Pelosi moja kwa moja amemlaumu raisTrump kwa kuchochea alichoita uasi wa kutumia nguvu dhidi ya Marekani.
Spika Pelosi na kiongozi wa maseneta wa chama cha Democrats Chuck Schumer walijaribu kuwasiliana kwa njia ya simu na makamu wa rais Mike Pence kumtaka achukue nafasi ya rais Trump mara moja kwa mujibu wa kipengele hicho cha 25 cha katiba ya Marekani kinachomruhusu makamu wa rais kuchukua hatua hiyo, ikiwa rais ameshindwa kuyatimiza majukumu yake.
Tazama:
Kufuatia sakata hilo la wafuasi wa Trump kulivamia bunge, washauri wengine wanne katika Baraza la Usalama wa Taifa katika ikulu ya Marekani wamejiuzulu. Shirika la habari la Reuters limeripoti juu kujiuzulu maafisa hao siku ya Alhamisi ambao ni Erin Walsh, mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya Afrika, Mark Vandroff mkurugenzi mwandamizi wa sera ya ulinzi, Anthony Rugierro, mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya silaha za maangamizi na Rob Greenway mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Chanzo:/AP/RTRE