Marekani na UN kushinikiza misaada kuingia Tigray
30 Julai 2021Haya yanakuja wakati ambapo kuna hofu kuwa mamilioni ya watu wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula.
Power anatarajia kukutana pia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye amedai kuwa hakuna njaa Tigray pamoja na maafisa waandamizi wanaovilaumu vikosi vya majeshi ya Tigray kwa misaada kutoingia eneo hilo. Majeshi ya Tigray yamechukua tena udhibiti wa sehemu kubwa ya jimbo hilo na wameapa kupambana na maadui zao hata walio nje ya mipaka.
Lakini afisa mmoja wa USAID ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa madai ya serikali ya Ethiopia kwamba majeshi ya Tigray ndiyo ya kulaumiwa kwa misaada kutoingia eneo hilo, ni uongo mtupu huku akisema kizingiti kikuu ni serikali ya Ethiopia. Afisa huyo hakutaka kutambulishwa kwa kuwa hakuwa na mamlaka ya kulizungumzia suala hilo ila mashuhuda wanasema hilo ndilo tatizo kubwa Tigray kwa miezi sasa.
Watu milioni 5.2 Tigray wanategemea misaada ya nje ya nchi
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba huenda misaada ya chakula ikaisha katika siku chache zijazo katika mji mkuu wa Tigray Mekele iwapo misaada zaidi haitokubwaliwa kuingia. Babar Baloch ni msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wakimbizi UNHCR.
"Hakuna maji safi ya kunywa, hakuna huduma za afya na njaa ni hatari kubwa. Usambazaji wa mwisho wa chakula kwa kambi zote za wakimbizi ulifanyika mwishoni mwa mwezi Juni na chakula cha mwezi mmoja tu ndicho kilichotolewa," alisema Baloch.
Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 5.2 ambao ni zaidi ya asilimia 90 ya wakaazi wa Tigray wanategemea misaada ya kutoka nje ya nchi.
Samantha power kuelekea Sudan pia
Mapema mwezi huu msafara wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa WFP ulivamiwa na sasa njia zote za kuingia Tigray zimekatwa kutokana na vizuizi au hofu ya usalama.
Kulingana na USAID, katika ziara yake itakayoanza hapo Jumamosi, Power, atasafiri pia kuelekea Sudan wakati ambapo mataifa ya Magharibi yanatafuta kuiunga mkono serikali ya mpito ya Sudan inayoungwa mkono na raia baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kiimla.
Waziri mkuu wa Sudan Abdulla Hamdok analenga kufikisha mwisho mapigano katika nchi hiyo ikiwemo mapigano ya Darfur ingawa mapigano mapya katika miezi ya hivi karibuni yamesababisha vifo vya mamia ya watu.