1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawaondoa wafanyakazi wake Lahore

9 Agosti 2013

Saudi Arabia imesema imewakamata watu wawili wanaoshukiwa kuwa wanachama wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda waliopanga kufanya mashambulizi ya kigaidi kwenye balozi za mataifa ya Magharibi katika Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/19Mn9
Waziri wa kigeni wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Saudi Arabia, Prince Saud al-Faisal
Waziri wa kigeni wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Saudi Arabia, Prince Saud al-FaisalPicha: Jacquelin Martin/AFP/Getty Images

Ama kwa upande mwingine, Marekani imewaondoa wafanyakazi wake katika ubalozi mdogo wa Lahore, Pakistan kutokana na kitisho cha kushambuliwa kwa ubalozi huo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia imesema kuwa watu hao wawili waliokamatwa na ambao ni raia wa Yemen na Chad, wana mawasiliano na Tawi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaida katika Rasi ya Uarabuni, AQAP.

Msemaji wa wizara hiyo, Jenerali Mansour al-Turki amesema kuwa mtuhumiwa mwenye uraia wa Chad alifukuzwa Saudi Arabia, lakini alirejea kwa kutumia hati ya kusafiria iliyotolewa na nchi nyingine.

Kiongozi wa AQAP, Nasser al-Wahaishi
Kiongozi wa AQAP, Nasser al-WahayshiPicha: picture-alliance/dpa

Al-Turki amesema kuwa watu hao wawili wanahusishwa na vitisho vilivyotolewa dhidi ya balozi za mataifa ya Magharibi katika Mashariki ya Kati.

Tishio hilo lilisababisha kufungwa kwa balozi za Marekani na washirika wake wa mataifa ya Magharibi kwenye eneo la Mashariki ya Kati, Asia na Afrika. Kundi la AQAP liliundwa mwaka 2009 kama tawi kuu la Al-Qaeda nchini Yemen na Saudi Arabia na linaongozwa na Nasser al-Wuhayshi.

Wafanyakazi ubalozi mdogo wa Marekani, Lahore waondolewa

Kukamatwa kwa watu hao kumetokea wakati ambapo Marekani imewaondoa wafanyakazi wake katika ubalozi mdogo wa Lahore, Pakistan kutokana na kuwepo vitisho vya kushambuliwa ubalozi huo.

Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Islamabad, Meghan Gregonis, amesema kuondolewa kwa wafanyakazi hao hakuhusiani na vitisho vya awali vilivyosababisha kufungwa kwa balozi za nchi hiyo Mashariki ya Kati na Afrika.

Maafisa wa usalama wa Pakistan, wakiulinda ubalozi mdogo wa Marekani, Lahore
Afisa wa usalama wa Pakistan, akiulinda ubalozi mdogo wa Marekani, LahorePicha: PakistanPakistanArif Ali/AFP/Getty Images

Marekani pia imewaonya raia wake kutokwenda Pakistan. Gregonis amesema kuwa wafanyakazi hao wanapelekwa mjini Islamabad.

Wakati hayo yakijiri, Yemen, imeripoti kuongezeka kwa mashambulio ya ndege za Marekani zisizo na rubani.

Kwa mujibu wa duru za kijeshi, wanamgambo 12 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Al-Qaeda wameuawa katika mashambulio ya jana Alhamisi (08.08.2013). Mauaji hayo, yanafanya idadi ya wanamgambo waliouawa katika muda wa wiki mbili zilizopita, kufikia kiasi 34.

Yemen yaangaliwa kwa makini

Yemen imekuwa ikiangaliwa kwa jicho pana la dunia kutokana na tishio hilo la kufanyika mashambulizi ya kigaidi. Tishio hilo, lilisababisha Ujerumani, Marekani, Ufaransa na Uingereza, kuzifunga balozi zake mwishoni mwa juma lililopita.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa hatua ya kufungwa kwa balozi hizo, inatokana na kupatikana kwa ujumbe wa mawasiliano ya siri kati ya kiongozi wa Al-Qaeda, Ayman al-Zawahiri na kiongozi wa AQAP, Al-Wuhayshi kuhusu kupanga shambulio kubwa la kigaidi.

Ndege ya Marekani isiyo na rubani
Ndege ya Marekani isiyo na rubaniPicha: Reuters

Jarida la Wall Street Journal, limemnukuu afisa wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, akisema kwamba Al-Wuhayshi ndiye kinara wa mpango huo uliosababisha tahadhari duniani. Taarifa za awali zinaeleza kuwa Al-Wuhayshi aliamuriwa kufanya mashambulizi hayo na Al-Zawahiri.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Gakuba Daniel