1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Marekani yazitaka Rwanda, Kongo kuutuliza mvutano

16 Agosti 2023

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken amefanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kushinikiza kutulizwa kwa uhasama baada ya kuzuka mivutano mipya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4VFBQ
Marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda wakiwa kwenye picha ya pamoja
Marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi (Kushoto) na wa Rwanda Paul Kagame Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema Blinken alifanya mazungumzo muhimu ya simu na Kagame kuhusu hali tete kati ya Rwanda na Kongo, bila kuchukua msimamo wowote kuhusu madai ya uvamizi uliofanywa mpakani.

Jeshi la Kinshasa mwishoni mwa mwezi jana lilivituhumu vikosi vya Rwanda kwa kuingia katika eneo lake la mpakani, madai ambayo Kigali iliyakanusha.

Mazungumzo hayo yanajiri baada ya naibu wa Blinken, Victoria Nuland, kuzuru Kinshasa na kuujadili msuguano huo na Rwanda na Rais Felix Tshisekedi. Blinken amewasilisha ujumbe wa kupatikana suluhisho kupitia diplomasia kati ya nchi hizo mbili jirani.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani wakati alipozuru kanda hiyo mwaka jana alisema alipata madai ya kweli ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.

Kigali inakanusha madai hayo, lakini inataka hatua kuchukuliwa dhidi ya waasi wa Kihutu wa FDLR, wanaohusishwa na wahusika wa mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda