Rais Kagame afanya mabadiliko katika idara ya jeshi
7 Juni 2023Hayo yanajiri baada ya jana Rais Kagame kumteua waziri mpya wa ulinzi, mkuu wa majeshi na mkuu wa usalama wa ndani. Jeshi la Ulinzi la Rwanda limesema katika taarifa yake kuwa makamanda wawili wa ngazi ya juu wamefukuzwa kazi, pamoja na maafisa wengine zaidi ya watu 200 wenye vyeo mbalimbali. Meja Jenerali Aloys Muganga, na Brigedia Jenerali Francis Mutiganda wamefukuzwa pamoja na maafisa wengine 14.
Sababu za mabadiliko hazijajulikana
Muganga aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2019, na Mutiganda aliteuliwa kuwa mkuu wa usalama wa nje katika Idara ya Usalama na Ujasusi ya Rwanda, NISS hadi Oktoba, mwaka 2018, wakati aliporudishwa kwenye makao makuu ya Jeshi la Rwanda RDF na kupangiwa jukumu ambalo halikuwekwa wazi. Hata hivyo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kutokana na mabadiliko hayo.
Jana, Rais Kagame alitangaza kumteua Juvenal Marizamunda kuwa waziri wa ulinzi, akichukua nafasi ya Albert Murasira ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2018. Marizamunda, mwenye umri wa miaka 58 awali alikuwa mkuu wa idara ya magereza ya Rwanda na pia naibu wa inspekta jenerali wa polisi wa zamani.
Rais Kagame pia amemteua Mubarak Muganga kuwa mkuu mpya wa majeshi, na Vincent Nyakarundi kuwa mkuu wa majeshi ya ardhini. Jean Bosco Ntibitura ameteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa usalama katika Idara ya Usalama na Ujasusi ya Rwanda, NISS. Mabadiliko mengine yamefanyika kwa makamanda wa kikosi cha Rwanda ambacho kimepelekwa Msumbiji tangu mwaka 2021 kupambana na wapiganaji wa jihadi.
Wiki iliyopita, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo lililishutumu jeshi la Rwanda na kundi la waasi wa M23 kwa kupanga shambulizi kwenye mji wa Goma. Mara kwa mara Kongo imekuwa ikiishutumu jirani yake Rwanda kwa kuwaunga mkono M23, madai yanayoungwa mkono na nchi kadhaa za Magharibi na wataalamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo.
Mahakama ya Umoja wa Mataifa: Kabuga hawezi kusimama kizimbani
Wakati huo huo, majaji wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa afya ya mshtakiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Felicien Kabuga haimruhusu kusimama kizimbani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Uamuzi huo uliotangazwa Jumatano na majaji wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kesi ya Uhalifu, IRMCT unamaanisha kuwa Kabuga, mwenye umri wa miaka 88 kwa mujibu wa maafisa, ingawa mwenyewe anadai ana miaka 90, hakuna uwezekano wa kutiwa hatiani kwa sababu hana uwezo wa kiafya na kimwili kusimama kizimbani. Kwa mujibu wa majaji hao, badala ya kuiondoa kesi ya Kabuga mahakamani, wataandaa utaratibu mwingine wa kisheria kwani hawezi kushiriki tena kesi yake kikamilifu.
(AFP, AP, Reuters)