Mataifa 44 ya Ulaya yakutana ili kukabiliana na Urusi
6 Oktoba 2022Mkutano huo wa Prague ni wa uzinduzi wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC) na uliopendekezwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ili kuwaleta pamoja wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya na nchi zingine 17 za bara hilo. Baadhi ya mataifa yanasubiri kujiunga rasmi na Umoja huo huku Uingereza, ikiwa nchi pekee iliyowahi kujiondoa katika muungano huo.
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema wote waliopo katika mkutano huo wanafahamu kuwa shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine ni ukiukaji wa kikatili wa mfumo wa amani na usalama na kwamba hawatokubali kuona sehemu ya nchi jirani ikinyakuliwa kinyume cha sheria.
Kauli yake Scholz imeungwa mkono na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.
Mkutano wa kuashiria mshikamano
Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss, baada ya kukutana na mwenyeji wa mkutano huo ambaye ni Waziri Mkuu wa Czech Petr Fiala, amesisitiza "nguvu ya makubaliano yao juu ya umuhimu wa fikra ya pamoja kwa demokrasia ili Ulaya kuwasilisha msimamo wa pamoja dhidi ya kile alichokiita ukatili wa Putin".
Soma zaidi: Mkutano wa viongozi wa mataifa ya Ulaya mjini Prague kutuma ishara wazi kwa Urusi
Mkutano wa Prague unachukuliwa kama ishara ya mshikamano wa nchi za bara la Ulaya, ambazo zinakabiliwa na migogoro lukuki, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa usalama kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine, mgogoro wa kiuchumi na hata ule nishati.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa anatarajia kuwa watafikia makubaliano ya pamoja: "Kwanza kabisa, ni kuonyesha umoja wetu. Na pia, kwa mataifa yote ya Ulaya, iwe ni wanachama wa EU au la, ni nafasi ya kuunda urafiki wa kimkakati na tuwe na uelewa sawa juu ya matatizo yanayolikumba bara letu la ulaya."
Ukosefu wa hatua
Mbali na hotuba na kauli za kuvutia, kulikuwa na mashaka juu ya malengo rasmi na hatua madhubuti zitakazochukuliwa na viongozi hao. Waziri Mkuu wa Latvia Krisjanis Karins amesema hakuna maamuzi yoyote yaliyotarajiwa katika mkutano huo, huku akisisitiza kuwa lengo la msingi ni kushirikiana na kufanya kazi pamoja.
Soma zaidi:Umoja wa Ulaya wachukua hatua kukabiliana na kupanda kwa bei ya nishati
Wengine wanatilia mashaka ufanisi wa mkutano huo wa EPC na kusema itakuwa vigumu kufikia malengo, si kwa sababu tu ya ukubwa wake bali pia ushindani uliopo baina ya wanachama walio wengi, mfano wa Armenia na Azerbaijan au Ugiriki na Uturuki.
Nchi 27 za Umoja wa Ulaya zitaendelea mazungumzo hadi kesho Ijumaa, ili kujadili tofauti zao kuhusu jinsi ya kupunguza bei ya gesi ili kudhibiti kupanda kwa gharama za nishati ambazo zinaathiri ufufuaji wa uchumi baada ya janga la COVID-19.