Mataifa ya Afrika ya Kati yachukulia vipi mapinduzi Gabon ?
1 Septemba 2023Rais wa Congo-Brazzaville, Denis Sassou Nguesso alikuwa mwenyeji wa mwenzake wa Angola Joao Lourencou ambao walizungumzia mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon. Marais hao wamelaani kile walichokiita unyakuzi wa madaraka kwa nguvu. Sassou Nguesso na Lourencou wamewataka viongozi wa kijeshi kuhakisha usalama wa rais Bongo na familia yake. Rais wa Congo-Brazzaville anahusiano wa kipekee na Gabon. Mwanae aliolewa na Omar Bongo rais wa zamani wa Gabon na baba wa rais Ali Bongo. Congo-Brazzaville pia inagawa mpaka wa zaidi ya kilomita 1,900 na Gabon. Nchi hizo pia zina mila na tamaduni zinazofanana.
''Kisaikolijia watu wanashangilia''
Katika mitandao ya kijamii, watumiaji wengi wa Intaneti wa Kongo-Brazzaville wanahoji zamu yao itafika lini ? Hakika, kwa takriban miaka 40 madarakani, rais Denis Sassou-Nguesso ni mmoja wa marais wakongwe wa Kiafrika ambao bado wako madarakani, na nchini humo upinzani haupo kabisa.
Sadio Kanté-Morel, mchambuzi wa maswala ya kisiasa ya Kongo, amesema mapinduzi ya Gabon yanaibua wasiwasi kwa viongozi wa nchi jirani na kuamsha dhamira ya wananchi wake.
''Madhara kwa nchi jirani ya Kongo yatakuwepo. Kisaikolojia watu walishangilia kidogo wakidhani labda zamu ya Kongo ya mapinduzi itafika.'', alisema Sadio.
Aibu kwa viongozi wa nchi za Afrika ya Kati ?
Kwa upande wake, Parfait Moukoko, Mwenyekiti wa Almashauri ya mashirika za Haki za Kibinadamu nchini Kongo-Brazzaville, anasema mapinduzi ya Gabon yataleta ari mpya ya uongozi nchini mwake.
"Mapinduzi hayo yanatoa fursa kwa utawala uliopo kubadili utendaji wake kisiasa, kuuboresha mapungufu yake na ni somo kutoka kwa kile kinachotokea Gabon na kwingineko. Wanatakiwa kurejesha demokrasia ya kweli na kuandaa uchaguzi wa wazi nchini Kongo-Brazza.'',alisema Moukoko.
Moukoko amesema ukimya wa viongozi wa Kongo-Brazzaville kufuatia mapinduzi ya Gabon, unatokana na aibu walionayo kuhusu uongozi uliofanana na nchi hiyo jirani. Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia hali nchini Gabon inafuatiliwa kwa umakini na wananchi pamoja na viongozi.
Hata hivyo mbunge wa chama tawala, Steve Mbikayi alisema mapinduzi ya Gabon hayawezi kuchukuliwa kama mkwamo wa kidemokrasia kwa sababu Bongo na familia yake wameiongoza nchi hiyo kwa miaka 56 na hiyo ni aibu kwa bara zima la Afrika. Wabunge wengine mjini Kinshasa pia wamechukua tukio la mapinduzi ya Gabon kukumbusha umuhimu wa kuwepo na taifa la haki.
Huko Gabon kwenyewe, kiongozi wa upinzani amesema mapinduzi ya Jumatano ni njama ya familia ya rais Bongo yakuendelea kushikilia madaraka.