1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Magharibi yatoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine

20 Aprili 2022

Urusi imetoa muda mwingine wa mwisho kwa wapiganaji wa Ukraine kujisalimisha Mariupol wakati ikizidisha mashambulizi yake maeneo ya mashariki mwa Ukraine huku serikali za Magharibi zikitoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine

https://p.dw.com/p/4A8l7
Peru Lima Protest Botschaft Russland
Picha: Carlos Garcia Granthon/Zuma/picture alliance

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov amesema Urusi imeendeleza usiku kucha mashambulizi ya anga na kuyalenga maeneo 73 ya kijeshi nchini Ukraine, na kuwaua hadi askari 40 wa jeshi la Ukraine pamoja na magari saba ya kivita kuharibiwa. Hata hivyo, habari hii haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Wakati huo huo, Ukraine leo imepokea ndege mpya za kijeshi kutoka kwa mataifa washirika kusaidia kuimarisha uwezo wake wa kujilinda wakati ambapo Urusi inazidisha mashambulizi upande wa mashariki ikilenga kulikamata jimbo la Donbas.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imethibitisha kupelekwa kwa ndege za kivita nchini Ukraine lakini haikutaja idadi wala mataifa yaliyochangia msaada huo wa kijeshi. 

soma zaidi: Charles Michel yupo ziarani Ukraine

Serikali mjini Kyiv iliyaomba mataifa ya Magharibi kuipatia ndege aina ya MiG chapa 29s kwa sababu marubani wake wana uzoefu wa kuzirusha na mataifa mengi ya mashariki mwa Ulaya yanamiliki ndege hizo. Uamuzi wa kuipatia Ukraine ndege za kivita ni sehemu ya juhudi za hivi karibuni kabisa za mataifa ya Magharibi kujibu operesheni kali inayofanywa na Urusi.

Serikali ya Norway imesema leo kuwa imeipatia Ukraine takriban makombora 100 aina ya Mistral yaliyotengenezwa na Ufaransa na yenye uwezo wa kudungua ndege. 

Zelenskyy aomba silaha zaidi

Ukraine | Der ukrainische Präsident Wolodymyr Selenskyj
​​​​Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: AFP

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema jeshi la Ukraine lina ubora ispokuwa wana uhaba wa silaha. "Laiti tungekuwa na silaha zote tunazohitaji, ambazo washirika wetu wanazo na ambazo zinalinganishwa na silaha zinazotumiwa na Urusi, tungekuwa tayari tumemaliza vita hivi. Tungelikuwa tayari tumerejesha amani na kukomboa eneo letu kutoka kwa wavamizi. Kwa sababu ubora wa jeshi la Ukraine katika mbinu na hekima ni dhahiri kabisa."

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk amesema leo kuwa Ukraine imefikia makubaliano mapya na Urusi juu ya kuanzisha njia za kiutu ili kuwahamisha wanawake, watoto na wazee kutoka mji uliozingirwa wa Mariupol kutokana na hali mbaya ya kibinadamu huko Mariupol.

soma zaidi: Vita vya Ukraine vyautikisa uchumi wa dunia - IMF

Mamlaka zimesema maelfu ya watu wameuawa kutokana na kuzingirwa kwa Mariupol na kwamba katika mji huo wa bandari kwenye Bahari ya Azov umeharibiwa kabisa.

Makubaliano ya awali ya kuanzisha njia za kiutu ili kufaanikisha zoezi la raia kuondoka Mariupol yalivunjika mnamo Machi 5. Tangu wakati huo, juhudi za mara kwa mara za kuanzisha njia za kiutu zimekuwa zikigonga mwamba, huku pande zote mbili zikitupiana lawama.

Vyanzo: RTRE, DPA, AFP