Mataifa yajipanga kulazimisha chanjo ya corona kwa wote
16 Desemba 2021Makadirio kwamba aina hiyo ya kirusi cha Covid-19 kilichoobadilika na kinachoambukiza kwa haraka yanaweza kuwa makubwa katika Umoja wa Ulaya mapema mwezi ujao, yamepelekea suala hilo kuwekwa juu kabisa katika ajenda ya mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya unaoendelea mjini Brussels na kuzua hofu ya kuzuka kwa janga la kiafya.
Ulaya inajiandaa kwa majira ya baridi na kitisho cha Omicron, huku Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen akisema kuwa Omicron itakuwa imesambaa kote barani Ulaya ifikapo mwezi Januari.
"Kinachonitia wasiwasi ni kwamba tunaona Omicron ikisambaa, aina hii mpya ya kirusi inaonekana inaambukiza zaidi. Tunaambiwa na wanasayansi kwamba kufikia katikati ya Januari, tunapaswa kutarajia Omicron kuwa aina mpya ya kirusi itakayokuwa imeenea barani Ulaya." Alisema von der Leyen.
Ingawa nchi nyingi za Umoja wa Ulaya ziko katika mstari wa mbele kimataifa katika suala la viwango vya chanjo, ugavi huo hauko sawa katika mataifa yote 27 ya Umoja huo. Nchi tisa za Umoja wa ulaya zina viwango vya chanjo chini ya asilimia 60.
Ufaransa, Israel, Ghana zachukuwa hatua kali
Serikali ya Ufaransa ilisema kuanzia Jumamosi (18 Disemba) ingelipiga marufuku safari zisizo za lazima kwenda na kutoka Uingereza ili kupunguza kasi ya kuenea kwa Omicron, na hatua hiyo itawalenga waliochanjwa na ambao bado.
"Wafaransa watakaotaka kwenda Uingereza watalazimika kutoa sababu muhimu na hawatoweza kusafiri kwa sababu za kitalii au za kitaaluma," serikali ilisema katika taarifa yake, na kuongeza kuwa raia wa Ufaransa na raia wa Umoja wa Ulaya bado wanaweza kurejea Ufaransa kutoka Uingereza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett alisema siku ya Jumatano (Disemba 15) kuwa Israel ingeliendeleza hatua ya kufunga mipaka yake hadi mwishoni mwa mwezi Disemba ili kuzuia kuenea kwa Omicron.
Hatua kama hiyo imechukuliwa pia na Ghana ambayo imeanzisha vikwazo vipya vya usafiri nchini humo. Sasa watu wanaweza tu kuingia katika taifa hilo la Afrika Magharibi kwa kupitia angani au baharini; na mupaka ya ardhini imepigwa marufuku kwa muda usiojulikana.
Nchini Afrika Kusini kulikogundulika Omicron kwa mara ya kwanza, Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Virusi vya Corona limechukua hatua za uangalifu katika kukabiliana na kusambaa kwa kirusi hicho, na kuagiza idara hiyo kufuatilia kwa karibu kuongezeka kwa maambukizo, idadi ya waliolazwa hospitalini na viwango vya vifo na waliopona Covid-19.