1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yenye nguvu duniani yanakutana Ufaransa

12 Novemba 2021

Mataifa yenye nguvu duniani yanakutana Ufaransa kushinikiza ufanyike uchaguzi nchini Libya kufikia mwisho wa mwaka huu na pia kutilia mkazo juhudi za kuondoa majeshi ya kigeni katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

https://p.dw.com/p/42uwW
Internationale Libyen Konferenz
Picha: Mahmud Turkia/AFP/Getty Images

Hata hivyo, juhudi hizo zinatatizwa na kuongezeka kwa malumbano ya kisiasa yanayoweza kuurejesha nyuma mchakato wa amani ulioendeshwa kwa mwaka mzima. 

soma Miaka 10 tangu Gaddafi kuuawa, Libya ingali inayumba

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaogoza mkutano huo wa kimataifa mjini Paris unaolenga kuhakikisha kwamba Libya inashikilia mpango wake wa kufanya uchaguzi mnamo Disemba 24 na kufungua ukurasa mpya katika historia yake.

Makubaliano ya kuandaa uchaguzi huu yaliafikiwa chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa mwaka jana ambayo pia yalianzisha serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa kuchukua nafasi kutoka kwa serikali mbili pinzani za upande wa mashariki na magharibi, ambazo zimekuwa zikipigana kwa miaka mingi.

Soma Je Libya, itashindwa kufanya uchaguzi wa Desemba?

Kumaliza mzoto Libya

Frankreich | Emmanuel Macron und Kamala Harris
Picha: Christoph Ena/AP/picture alliance

Mchakato huo unaonekana kama nafasi ya kumaliza muongo mzima wa vita kufuatia ghasia za 2011 zilizoungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na viliyomng'oa madarakani Muammar Gaddafi na kuwa tishio kwa utulivu wa eneo zima la Mediterania.

Hata hivyo, kuna hofu iwapo pande zinazohasimiana zitayakubali matokeo ya uchaguzi, na hivyo kuiweka tena Libya kwenye hatari ya mapigano mapya. Nchi hiyo imekuwa kituo kikuu cha kuwasafirisha wahamiaji wanaopania kuvuuka bahari ya Mediterenia na kuingia Ulaya.

Takriban nchi na mashirika 30 yanatarajiwa kuhudhuria mkutao huo mjini Paris, ikijumuisha majirani wa Libya, na nchi ambazo zimegawanyika juu ya mzozo huo.

Viongozi watakaohudhuria

Libyen Premierminister Abdul Hamid Mohammed
Abdul Hamid Mohammed Dbeibah Picha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo wa leo ni makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris pamoja na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.

Libya itawakilishwa na Mohamed al-Menfi, mkuu wa baraza la mpito ambalo ndilo linalotekeleza majukumu ya mkuu wa nchi kabla ya uchaguzi, pamoja na Waziri Mkuu Abdelhamid Dbeibah.

Awali Paris ililenga kwamba viongozi wakuu wa Uturuki na Urusi wangehudhuria mkutano huo lakini Ankara na Moscow wametuma wawakilishi wa ngazi za chini.

Mamluki kutoka kampuni ya ulinzi ya Urusi ya Wagner inayoshirikiana pamoja na Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) lenye makao yake mashariki mwa Libya wanaungwa mkono na Moscow, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri.

soma Umoja wa Ulaya wataka wapiganaji mamluki kuondoka Libya

Vikosi vilivyoko mashariki mwa Libya vilisema Alhamisi kuwa vimekubali kuwarejesha mamluki 300 wa kigeni kutoka katika eneo lao la udhibiti baada ya ombi kutoka Ufaransa.

 

Vyanzo: Reuters/AFP